Rais wa Venezuela amkejeli Trump, asema amemfanya mashuhuri
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ametumia kinaya kumkejeli Donald Trump na kusema kuwa rais huyo wa Marekani amemfanya awe shakhsia maarufu duniani.
Akiongea jana Jumapili kupitia televisheni ya serikali baada ya kurejea nchini akitokea Russia, Belarus na Uturuki, Maduro amemshukuru Trump kwa 'kumkosoa' na 'kumtaja' kila siku, jambo ambalo anasema limempa umashuhuri kote duniani.
Huku akizungumza kwa tabasamu na vicheko vya kejeli, Rais wa Venezuela amesema: "Ni fahari kubwa kwamba 'mfalme wa dunia' ananitaja kila siku, hilo linaonyesha kuwa nafanya jambo lililo sawa."
Rais Maduro amemkejeli zaidi rais huyo wa Marekani kwa kusema : "inaelekea Trump amegeuka na kuwa kiongozi wa upinzani hapa nchini. Kadri anavyonikosoa au kunipaka matope ndivyo anafanya nizidi kujulikana na kupendwa zaidi duniani."
Hivi karibuni, Venezuela ilisema Marekani inaendeleza 'ugaidi wa kisaikolojia' dhidi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini, huku ikimtaka Rais Donald Trump kuwa mtu anayejifanya 'bepari wa dunia', ikiwa ni radiamali ya Caracas baada ya Washington kuijumuisha Venezuela katika orodha ya nchi nane ambazo raia wao wamepigwa marufuku kuingia Marekani.
Maduro ameongeza kuwa, Venezuela inatathmini kuanza kutumia sarafu za yuro, yen na rupee badala ya dola katika mabadilishano yake ya kibiashara.