Msichana mdogo Muislamu ashambuliwa kutokana na Hijabu yake nchini Canada
-
Khawlah Noman akihojiwa na vyombo vya habari
Polisi wa mjini Toronto Canada wametangaza habari ya kushambuliwa binti mmoja mdogo Muislamu kutokana na kuvaa Hijabu.
Kwa mujibu wa polisi hao, mtu mmoja mwenye chuki za kidini aliichana kwa mkasi Hijabu ya msichana huyo mjini Toronto na baadaye kukimbia.
Msichana huyo mdogo Musilamu, Khawlah Noman, mwenye umri wa miaka 11 amehojiwa na televisheni za eneo hilo na kusema kuwa, mtu huyo alianza kumtukana kwanza kabla ya kumvamia na kumchania Hijabu yake. Hata hivyo kwa mujibu wa polisi ya Toronto, msichana huyo Muislamu hakujeruhiwa kimwili.
Kwa upande wake Kathleen O'Day Wynne, waziri kiongozi wa jimbo la Ontario ambalo makao yake makuu ni Toronto amelaani kitendo hicho na kusema ni kiovu sana na kimetokana na chuki.
Matamshi hayo yametolewa katika hali ambayo kabla ya hapo kulikuwa kumeripotiwa habari kwamba maadui wa Uislamu hivi karibu waliufyatulia risasi msikiti wa Quebec nchini Canada na kuua Waislamu watano na kujeruhiwa wengine wengi.
Kabla ya hapo pia, jimbo la Quebec nchini Canada lilikuwa limepaisha sheria za kuwapiga marufuku wanawake Waislamu kuvaa niqab, yaani Hijabu inayofunika uso mzima wakiwa wanatumia huduma za umma.
Aidha mwaka 2015, msikiti mmoja katika jimbo la Ontario nchini Canada uliteketezwa kwa moto na watu wenye misimamo ya kurufutu ada wanaouchukia Uislamu.