Umashuhuri wa Rais na Waziri Mkuu wa Ufaransa wazidi kuporomoka
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa Ufaransa yanaonyesha kupungua uungaji mkono wa wananchi kwa Rais na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Taasisi ya Ifop ya nchini Ufaransa iliyofanya uchunguzi huo wa maoni imebainisha kuwa, uungaji mkono wa wananchi kwa Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo katika kipindi cha mwezi mmoja yaani kati ya tarehe tisa hadi 17 mwezi huu wa Machi umepungua kwa asilimia mbili na kufikia asilimia 42.
Taasisi hiyo ya uchunguzi wa maoni imesisitiza kuwa kiwango cha uungaji mkono wa wananchi kwa Waziri Mkuu wa Ufaransa, Edouard Philippe pia kimefikia asilimia 43 na kwamba kimepungua kwa asilimia tatu katika muda wa mwezi mmoja. Taasisi ya Ifop iliyofanya utafiti huo mpya wa maoni huko Ufaransa imetangaza kuwa asilimia 57 ya watu walioshiriki katika utafiti huo wameeleza kutoridhishwa na utendaji wa Rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron.
Uungaji mkono wa wananchi kwa Rais wa Ufaransa ulikuwa wa asilimia 55.
Hii ni mara ya tatu mtawalia ambapo kunashuhudiwa kupungua kiwango cha uungaji mkono wa wananchi wa Ufaransa kwa Rais na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.