Matamshi ya Rais wa Uturuki dhidi ya Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i42830-matamshi_ya_rais_wa_uturuki_dhidi_ya_ufaransa
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, kwa mara nyingine tena ameishutumu Ufaransa kuwa inawachochea magaidi kufanya jinai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 08, 2018 22:03 UTC
  • Matamshi ya Rais wa Uturuki dhidi ya Ufaransa

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, kwa mara nyingine tena ameishutumu Ufaransa kuwa inawachochea magaidi kufanya jinai.

Erdogan amesema hayo mbele ya wafuasi wa chama chake huko Denizli, kusini magharibi mwa Uturuki na kuongeza kuwa: Hatua ya Ufaransa ya kuwakaribisha magaidi katika Ikulu ya Elize ina maana ya kuwachochea magaidi hao kufanya jinai.

Shutuma hizo za rais wa Uturuki kwa serikali ya Ufaransa zimetolewa katika hali ambayo viongozi wa serikali ya Ankara katika siku za hivi karibuni wamekuwa mara kwa mara wakitoa shutuma kama hizo dhidi ya serikali ya Paris hasa baada ya kuzuka suala la kuondolewa wanajeshi wa Marekani nchini Syria na nafasi yake kupangwa kuchukuliwa na wanajeshi wa Ufaransa.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

 

Kwa mfano, wiki iliyopita, Fikri Işık, Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki aliishutumu serikali ya Ufaransa kuwa inashirikiana na kundi linalojulikana kwa jina la Vikosi vya Kulinda Wananchi (YPG). Katika upande mwingine, Ufaransa imekuwa daima ikiilaumu Uturuki kwa kuivamia kijeshi ardhi ya kaskazini mwa Syria katika operesheni yake ya kijeshi inayojulikana kwa jina la Tawi la Mzaituni. Pamoja na hayo tunaweza kusema kuwa, msuguano uliojitokeza baina ya Ankara na Paris umepata nguvu zaidi baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuonana siku ya Ijumaa ya tarehe 30 Machi 2018 na ujumbe wa wabunge wa Syria wakiwemo wa chama cha YPG na chama cha PYD na Paris kutangaza kuwa inaunga mkono juhudi za kurejesha utulivu kaskazini mwa Syria.

Itakumbukwa kuwa serikali ya Ankara imeingia kijeshi kaskazini mwa Syria na inaendelea na operesheni yake iliyoipa jina la Tawi la Mzaituni licha ya upinzani mkali uliooneshwa na sehemu kubwa ya wananchi wa Uturuki pamoja na viongozi wa vyama vya ndani ya nchi hiyo na vile vile upinzani mkubwa wa serikali halali ya Rais Bashar al Assad wa Syria na wa nchi nyingi za eneo hili.

Mara zote serikali ya Damascus imekuwa ikisema wazi kuwa uvamizi wa Uturuki katika mji wa Ifrin wa kaskazini mwa Syria ulioanza mwezi Januari mwaka huu wa 2018 ni uvunjaji wa wazi wa haki ya kujitawala ardhi nzima ya Syria. Kwa hakika licha ya viongozi wa Uturuki kuteka na kukalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya Syria lakini hawataki kulaumiwa kwa uvamizi wao huo. Serikali ya Damascus inakihesabu kitendo hicho cha Uturuki kuwa ni dharau kwake na imewataka wanajeshi vamizi wa Uturuki waondoke mara moja katika ardhi yake. 

Wanajeshi wa Uturuki ndani ya ardhi ya Syria

 

Alaakullihaal, duru za kisiasa za eneo hili zina wasiwasi mkubwa na harakati za viongozi wa serikali ya Ordogan. Amma kuhusiana na vitendo visivyo sahihi vya viongozi wa serikali ya Ankara, Zia Yalmaz, mmoja wa wataalamu wa masuala ya kisiasa wa Uturuki anasema:

Viongozi wa serikali ya Ankara ambao wanahesabiwa kuwa ni miongoni mwa viongozi waliofeli katika suala la Syria, wanafanya juhudi za kuepusha kugawanyika Uturuki kupitia kujiingiza kijeshi katika ardhi ya Syria.

Matamshi ya mtaalamu huyo wa masuala ya kisiasa wa Uturuki yana maana kwamba, viongozi wa serikali ya Ankara wameingia kijeshi kaskazini mwa Syria kwa shabaha ya kuzuia kugawanyika vipande vipande ardhi ya Uturuki baada ya kufeli siasa zao za kutaka kuipindua serikali halali ya Syria, suala ambalo kwa mtazamo wa wataalamu wa mambo doa lake jeusi la aibu, haliwezi kufutika katika kipaji cha uso wa serikali ya hivi sasa ya Uturuki.