Viongozi mbalimbali waendelea kupinga mashambulizi dhidi ya Syria
Mashambulizi yaliyofanywa na Marekani, Ufaransa na Uingereza huko Syria yamekabiliwa na upinzani mkubwa barani Ulaya na huko Marekani.
Marekani, Ufaransa na Uingereza leo alfajiri zimeyashambulia baadhi ya maeneo huko Syria kwa kisingizio cha madai ya kufanyika shambulio la silaha za kemikali katika mji wa Douma karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus. Mashambulizi hayo yamekabiliwa na upinzani mkubwa kutoka maeneo mbalimbali duniani ikiwemo huko Ulaya na Marekani kwenyewe.
Rais Vladimir Putin wa Russia ametoa taarifa akikosoa mashambulizi hayo ya kijeshi la Marekani na waitifaki wake huko Syria na kuyataja kuwa ni uvamizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala ya nchi iliyo huru ambayo inaongoza mapambano dhidi ya ugaidi. Taarifa ya Rais Putin imeongeza kuwa, kushtadi mivutano huko Syria kuna athari kubwa katika uhusiano wa kimataifa na kutaifanya hali ya mambo huko Syria kuwa mbaya zaidi
Naye Spika wa Bunge la Russia (Duma), Vyacheslav Volodin pia amekosoa mashambulizi hayo ya Marekani na waitifaki wake huko Syria na kueleza kuwa: Hatua hiyo ya Marekani si tu itawashughulisha wananchi wa Syria pekee bali pia hata nchi za Ulaya na kuilekeza dunia vitani. Spika wa Bunge la Russia amekosoa hatua ya Marekani ya kuupuza Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa hatua hizo za Marekani zinapasa kusitishwa haraka iwezekanavyo, hii ni kwa sababu nchi hiyo imeishambulia kwa makombora nchi inayojitawala bila ya kuzingatia sheria za kimataifa.
Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Cuba imetoa taarifa na kuyataja mashambulizi dhidi ya Syria kuwa ni uvamizi na ya upande mmoja, yaiyolipuuza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kukiuka sheria za kimataifa.
Katika upande mwingine, televisheni ya CNN ya nchini Marekani imetoa uchambuzi wake kuhusu mashambulizi ya Marekani, Uingereza na Ufaransa huko Syria na kuyataja kuwa ni ushindi kwa serikali ya Syria. CCN imeeleza kuwa: Kikosi cha Jeshi la Anga cha Damascus kimefanikiwa kuyalenga baadhi ya makombora yaliyovurumishwa huko Syria na si kwamba uwezo wa jeshi la Syria umesambaratishwa na kuangamizwa.