Serikali ya Uswisi yakataa pendekezo la kupiga marufuku burqa
(last modified Wed, 27 Jun 2018 13:45:15 GMT )
Jun 27, 2018 13:45 UTC
  • Serikali ya Uswisi yakataa pendekezo la kupiga marufuku burqa

Serikali ya Uswisi imepinga kampeni zinazofanyika mashinani za kushinikiza marufuku ya nchi nzima ya vazi la burqa linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu nchini humo.

Baraza la mawaziri limetoa taarifa hii leo baada ya mkutano wake na kusema: "Serikali inafahamu athari za watu kufunika nyuso zao, lakini yeyote atakayemlazimisha mwanamke kufunua uso wake atakabiliwa na kifungo cha hadi miaka mitatu jela."

Limesema kadhia hiyo itaamuliwa na wananchi wenyewe katika kura ya maoni hivi karibuni, kwani tayari sahihi 100,000 zimekusanywa na vuguvugu lenye chuki dhidi ya Uislamu linaitwa "Yes to a Mask Ban" linaloshinikiza kura hiyo.

Mwaka jana Bunge la Juu la Uswisi linalofahamika kama The Council of State lilikataa kuunga mkono muswada wa kupiga marufuku vazi hilo ambao tayari ulikua umepata baraka kamili za Bunge la Chini mwezi Septemba mwaka 2016.

Austria ni nchi nyingine ya Ulaya iliyopiga marufuku vazi hilo la stara katika maeneo ya umma

Muswada huo wa kupiga marufuku uvaaji wa burqa nchini humo uliandaliwa na wabunge wa chama cha mrengo wa kulia cha Swiss People’s Party, na iwapo ungepasishwa na Bunge la Juu, wanawake wa Kiislamu nchini humo wasingeruhusiwa kuvaa vazi hilo la staha katika maneo ya umma.

Hii ni katika hali ambayo, hapo jana Jumanne Bunge la Seneti la Uholanzi lilipasisha muswada wa sheria inayopiga marufuku vazi la stara la burqa linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu nchini humo.

Nchi nyingine za Magharibi kama vile Denmark, Bulgaria, Canada, Ubelgiji na Ufaransa zimepiga marufuku vazi hilo la stara.

Tags