Wanafunzi wa Kiafrika wanaotuhumiwa kwa ugaidi wakamatwa Uturuki
Makumi ya wanafunzi wa Kiafrika hususan raia wa Somalia wamekamatwa nchini Uturuki, wakihusishwa na Shirika la Kigaidi la Fathullah FETO, linalodaiwa kuratibu na kutekeleza jaribio la mapinduzi lililofeli la mwaka 2016.
Polisi nchini humo imesema kuwa, wanafunzi 10 raia wa Somalia, watatu wa Djibouti, na wawili wa Guinea wamekamatwa wakituhumiwa kuwa wanachama wa kundi hilo la kigaidi.
Wanafunzi hao walikamatwa katika operesheni zilizofanyika katika mji mkuu Ankara na katika mikoa ya Kirikkale na Diyarbakir.
Aidha wafunzi kadhaa raia wa Syria na askari 13 wa zamu wamekamtwa katika msako huo, ambao pia ulifanyika katika maeneo ya Kayseri, Busra, na Sirnak.
Mwaka jana kiongozi wa harakati ya Jama'at Gülen ambaye pia ni mpinzani wa serikali ya Uturuki, alikadhibisha kuhusika kwa aina yoyote na mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli tarehe 15 Julai mwaka 2016 na kusema kuwa mapinduzi hayo ulikuwa mchezo wa Rais Recep Tayyip Erdoğan mwenyewe.
Kwa mara kadhaa Fethullah Gülen amekuwa akikadhibisha tuhuma hizo na kusisitiza kuwa, Erdoğan alibuni mapinduzi hayo kwa lengo la kuwakandamiza wapinzani wake.
Tangu kulipojiri mapinduzi hayo, serikali ya Ankara imewatimua kazi malaki ya watumishi wa umma, wakiwamo walimu wa vyuo vikuu, wafanyakazi wa serikali, polisi na majaji. Katika mapinduzi hayo karibu watu 250 waliuawa na wengine 2000 kujeruhiwa.