Indhari kali ya Ufaransa dhidi ya siasa za kibiashara za Trump
Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amekosoa siasa za kiuchumi zinazotekelezwa na Rais Donald Trump wa Marekani kuuhusu Umoja wa Ulaya.
Akikosoa siasa hizo amesisitiza kwamba, Umoja wa Ulaya hautoruhusu siasa zake za kibiashara zivurugwe na rais huyo wa Marekani. Indhari kali ya Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ufaransa imetolewa kufuatia vitisho vya kibiashara vilivyotolewa na Trump kuhusu Umoja wa Ulaya. Itakumbukwa kuwa, kabla ya kusafiri kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Magharibi (NATO) mjini Brussels, Ubelgiji Trump aliashiria tena katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter suala la nakisi ya uwiano wa kibiashara wa dola bilioni 151 kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya na kulalamikia vikali suala hilo. Aidha Trump alidai kwamba watu wa Ulaya wamekuwa wakinufaika katika biashara zao na Marekani kutokana na ushuru wa kiwango kidogo uliowekwa na serikali ya Washington.
Hii ni katika hali ambayo watu wa Ulaya pia wanaamini kwamba Marekani ndio inayonufaika zaidi kutokana na uhusiano wake wa kibiashara na kiuchumi na Umoja wa Ulaya na kwamba suala hilo halina usawa. Wakati huohuo watu wa Ulaya wana wasi wasi kwamba Trump anafanya njama ya kuyaunganisha masuala ya kibiashara na bajeti ya kijeshi ya Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO). Kuhusiana na suala hilo, Stefano Stefanini, mwakilishi wa zamani wa Italia katika muungano huo anasema: "Itakuwa tishio halisi kuyaunganisha masuala ya usalama na biashara. Iwapo hilo litathibiti basi suala hilo litapelekea kusambaratika NATO." Inafaa kuashiria kuwa, serikali ya Rais Donald Trump imeziongezea ushuru wa asilimia 10 hadi 25 bidhaa za chuma na alumini zinazoagizwa kutoka nchi za Ulaya, Canada, Mexico, China na Russia. Mkabala wake nchi hizo na katika hatua ya kujibu mapigo nazo zimeziwekea ushuru mkubwa wa kibiashara bidhaa zinazozalishwa nchini Marekani. Ukweli ni kwamba siasa za Trump katika miezi ya hivi karibuni, zimeibua wimbi la mivutano ya kibiashara katika uga wa kimataifa, kiasi cha kuifanya Benki Kuu ya Dunia kuonya juu ya uwezekano wa kutokea vita vya kibiashara kufuatia siasa za rais huyo wa Marekani. Misimamo ya Trump ya kuipa kipaumbele zaidi Marekani na maslahi yake binafsi, ndio imemfanya achukue hatua hizo zilizo kinyume na misingi ya jamii ya kimataifa na hata ya washirika wake wa Ulaya. Kuhusiana na suala hilo, Robert Molley, mjumbe wa zamani wa Baraza la Usalama wa Taifa nchini Marekani, anaamini kwamba hatua za upande mmoja za Rais Donald Trump zimeipelekea nchi hiyo kutengwa kimataifa.
Hali hiyo imebainika wazi zaidi baada ya Trump kuiondoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kwa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA na pia hatua yake ya kuzipandishia ushuru wa kibiashara nchi rafiki za karibu na Marekani. Upinzani wa ndani dhidi ya Trump kutokana na siasa zake za kibiashara nao unazidi kuongezeka. Mambo hayo ndio yamepelekea kuibuka wasi wasi kwamba, huenda kuendelea siasa hizo za kibiashara, kukasababisha ongezeko kubwa la gharama za uzalishaji katika sekta ya viwanda ya nchi hiyo. Warner Antowler, Muhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha British Columbia cha nchini Canada amezitaja stratijia za kiuchumi za Trump kuwa za kuweweseka na kusisitiza kwamba, vita vya kibiashara vya Marekani dhidi ya mataifa yenye uchumi mkubwa duniani, vitailetea madhara makubwa Marekani yenyewe. Aidha amesema kuwa, matokeo ya kiuchumi na siasa za vita vya biashara zitaikaba koo serikali ya Trump. Kwa hakika Trump hajafahamu kwamba hawezi kuirejeshea Marekani kile alichokitaja kuwa ni shughuli zilizoporwa, kwani uchumi wa dunia umejengeka juu ya maelewano ya kimataifa. Alaakullihal, indhari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa imetolewa kwa kuzingatia matokeo haribifu ya kuendelea kwa siasa hizo za upande mmoja za Trump. Hasa ikitiliwa maanani kwamba, siasa hizo zinapelekea kuongezeka mpasuko katika uhusiano wa kambi mbili muhimu na wakati huo huo kuendelea kutengwa zaidi Marekani, kimataifa.