Askofu Mkuu wa New York: Kashfa za ngono zinavunja imani ya watu kwa kanisa Katoliki
(last modified Fri, 14 Sep 2018 23:57:28 GMT )
Sep 14, 2018 23:57 UTC
  • Askofu Mkuu wa New York: Kashfa za ngono zinavunja imani ya watu kwa kanisa Katoliki

Askofu Mkuu wa New York nchini Marekani amezungumzia kashfa kubwa ya vitendo vya kuwanajisi watoto katika kanisa Katoliki na kusema kuwa, hali hiyo itaondoa imani ya watu kwa taasisi hiyo ya kidini.

Timothy M. Dolan amesema kuwa maafa ya kuwanajisi watoto yanayofanywa na makasisi na wachungaji wa kanisa Katoliki ni mithili ya kuvuja kwa mavuta ya petroli na kuchafua bahari na kwamba kwanza huwasibu wahanga na familia zao. Askofu Mkuu wa New York ameongeza kuwa, sehemu kubwa ya maafa ya kashfa za ngono za makasisi na wachungaji huonekana pale waumini wa kanisa hilo wanapowaambia maaskofu kwamba, "ni vigumu sana kuwaamini nyinyi". Ameongeza kuwa hii ni licha ya kwamba, kanisa limejengwa kwa msingi wa imani ya watu na si kwa mabavu na ubabe.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa kanisa Katoliki amesema kuwa, mojawapo ya njia zinazoweza kurejesha imani ya watu kwa kanisa hilo ni kuruhusu polisi na mahakama kufanya uchunguzi kuhusu kashfa za vitendo vya kuwanajisi watoto wa waumini wa kanisa hilo. 

Askofu Mkuu wa New York, Timothy M. Dolan 

Kufichuliwa kwa kashfa kubwa ya vitendo vya makasisi na wachungaji vya kuwanajisi watoto na waumini wa kanisa Katoliki katika nchi kama Marekani, Ufaransa, Chile, Australia, Uholanzi, Ujerumani, Ufilipino na Italia kumezusha wasiwasi mkubwa baina ya wafuasi wa kanisa hilo. 

Uchunguzi uliofanywa nchini Ujerumani pekee umebaini kuwa zaidi ya watoto 3700 wamefanyiwa ukatili wa kingono katika makanisa ya nchi hiyo. 

Tags