Nov 14, 2018 14:21 UTC
  • Bangladesh yatumia askari kuwafukuza kwa nguvu wakimbizi Warohingya

Serikali ya Bangladesh imetuma maafisa usalama wakiwemo wanajeshi na askari polisi katika kambi za wakimbizi Waislamu wa Rohingya katika eneo la Cox wilayani Bazar, kusini mashariki mwa nchi kwa lengo la kuwafukuza kwa nguvu wakimbizi hao na kuwarejesha Myanmar.

Gazeti la Uingereza la The Guardian limeripoti leo kuwa, limeshuhudia kanda ya video inayoonesha maafisa hao usalama wa Bangladesh wakiwa wamezingira kambi za wakimbizi za Chakmarkul, Jamtoli na Hakimpara huku wakiwafanyia vitendo vya udhalilishaji wakimbizi hao Waislamu, ambao wataanza kurudishwa nchini kwao kwa nguvu kuanzia kesho Alkhamisi.

Hii ni katika hali ambayo, Jumatatu ya juzi, Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa aliitaka serikali ya Bangladesh kusimamisha mpango wake huo wa kuwarejesha kwa nguvu nchini Myanmar maelfu ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya akisisitiza kuwa maisha yao yatakuwa hatarini.

Amesema Bangladesh inapaswa kuangalia upya uamuzi wake wa kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi 2,200 wa Kirohingya nchini Myanmar kwani mazingira ya kuwapokea hayajaandaliwa.

Wakimbizi Waislamu wa Rohingya nchini Bangladesh

Kwa mujibu wa UN, zaidi ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya 700,000 wamekimbilia nchini Bangladesh tangu Agosti mwaka jana 2017, baada ya wanajeshi wa Myanmar wakishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali kuanzisha wimbi jipya la mauaji na hujuma dhidi ya Warohingya katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar.  

Mwezi uliopita, wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaoishi kambini nchini India walisema afadhali wauawe wakiwa ndani ya nchi hiyo badala ya kurejeshwa nchini kwao Myanmar.

Tags