Shughuli za serikali ya Marekani Zaendelea kukwama, Trump hana Krismasi
Sehemu kubwa ya shughuli za serikali ya Marekani zitaendelea kusitishwa kwa siku tano, kutokana na mkwamo kwenye ufadhili wa ujenzi wa ukuta wa kuzuia wahajiri katika mpaka wa Marekani na Mexico.
Kutokana na kusitishwa kwa shughuli za serikali, ambako kumeshuhudia baadhi ya mashirika mengi ya kiserikali yakisitisha operesheni zake siku ya Jumamosi (Disemba 22), Rais Donald Trump amesema atasalia mjini Washington katika sikukuu za Krismasi badala ya kwenda likizo mjini Florida.
Trump ameendelea kushinikiza juu ya kutengwa bajeti ya Dola bilioni 5 kuujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico lakini chame cha upinzani cha Democratic kinapinga vikali suala hilo. Hali hiyo imepelekea pande mbili kushindwa kufikia makubaliano ya kuendelea kuipatia fedha serikali kuendesha shughuli zake kikamilifu. Kwa msingi huo wafanyakazi 800,000 wa Idara ya Ulinzi wa Ndani, Usafiri na idara nyingine zimeathiriwa na kufungwa kwa serikali.
Kwa mujibu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Serikali ya Marekani, watu 420,000 ambao wanatambulika kuwa ni “muhimu” itawalazimu kufanya kazi bila ya malipo, wakati watu wengine 380,000 hawataweza kuripoti kazini kabisa. Kuna uwezekano mkubwa mkwamo huo ukaendelea hata baada ya mwaka mpya na hivyo kuitumbukiza Marekani katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiuchumi.