Mamilionea wa Marekani wasema hawataunga mkono kampeni za Trump 2020
Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la habari la CNBC unaonesha kuwa Rais Donald Trump wa Marekani anaendelea kupoteza uungaji mkono sio tu miongoni mwa wananchi, bali pia miongoni mwa wafanyabiashara matajiri waliomuunga mkono katika kampeni zake za uchaguzi uliopita mwaka 2016.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 34 tu ya mamilionea nchini Marekani ndiyo wameonesha kuwa watamuunga mkono Trump katika uchaguzi ujao wa rais wa mwaka 2020, ikilinganishwa na asilimia 45 mwaka jana.
Asilimia 54 ya mamilionea wa chama cha Democrats wamesema jambo wanalolipa kipaumbele ni kuhakikisha kuwa wanamuodoa Trump katika Ikulu ya White House.
Hata hivyo kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 62 ya mamilonea wa chama cha Republican cha Trump wameshikilia kuwa watasimama na rais huyo, katika uchaguzi huo wa 2020.
Asilimia 38 ya Wademocrats walioshirikishwa kwenye utafiti huo wa CNBC wanaamini kuwa, Makamu wa Rais wa zamani, Joe Biden ataibuka mshindi katika kura za mchujo wa chama hicho, na hivyo kuchuana na Trump katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020.