Ujerumani yapinga kuwekwa silaha za nyuklia za Marekani katika ardhi yake
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50449-ujerumani_yapinga_kuwekwa_silaha_za_nyuklia_za_marekani_katika_ardhi_yake
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema kuwa Berlin inapinga suala la kuwekwa silaha za masafa ya kati za nyuklia za Marekani katika ardhi yake.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 27, 2018 02:55 UTC
  • Ujerumani yapinga kuwekwa silaha za nyuklia za Marekani katika ardhi yake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema kuwa Berlin inapinga suala la kuwekwa silaha za masafa ya kati za nyuklia za Marekani katika ardhi yake.

Heiko Maas amesema kuwa, iwapo mkataba wa miaka 30 wa silaha za nyuklia za masafa ya kati wa INF baina ya Marekani na Russia ambao unapiga marufuku utumiaji wa makombora ya aina hiyo utavunjika, basi Ujerumani haitakubali kuwekwa silaha mpya za nyuklia za Marekani katika ardhi yake. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesisitiza kuwa, Ulaya haipaswi kuwa uwanja wa mivutano juu ya suala la kupanuliwa na kustawishwa zaidi silaha za nyuklia.

Mkataba wa INF unaizuia Marekani kuweka makombora ya nyuklia ya masafara ya kati barani Ulaya.

Ujerumani imechukua msimamo huo baada ya Marekani kutangaza hivi karibuni kwamba, itajiondoa katika mkataba wa silaha za nyukli za masafa ya kati (INF) ambao hadi sasa umeizuia Washington kuweka silaha za aina hiyo barani Ulaya.

Mkataba huo wa INF ulitiwa saini na viongozi wa Marekani na Urusi ya zamani mwaka 1987 na ulikuwa hatua muhimu sana katika kupunguza mizozano ya kipindi cha Vita Baridi.