Ripoti: Aghalabu ya Wamarekani wanataka Trump auzuliwe
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50493-ripoti_aghalabu_ya_wamarekani_wanataka_trump_auzuliwe
Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la Harvard CAPS kwa ushirikiano na taasisi ya utafiti ya Harris umeonesha kuwa akthari ya Wamarekani wanataka Rais Donald Trump wa nchi hiyo auziliwe au avuliwe madaraka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2018 04:42 UTC
  • Ripoti: Aghalabu ya Wamarekani wanataka Trump auzuliwe

Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la Harvard CAPS kwa ushirikiano na taasisi ya utafiti ya Harris umeonesha kuwa akthari ya Wamarekani wanataka Rais Donald Trump wa nchi hiyo auziliwe au avuliwe madaraka.

Ripoti ya utafiti huo iliyochapishwa na gazeti la The Hill jana Ijumaa imebainisha kuwa, asilimia 60 ya wapiga kura nchini Marekani wanadhani kuwa Trump anapaswa kuchukuliwa aina fulani ya hatua. 

Asilimia 39 ya watu walioshirikishwa kwenye utafiti huo wanasema Kongresi ya Marekani inapaswa kumvua madaraka Trump, wakati huu ambapo chama cha Democrats kinajiandaa kuchukua uongozi wa Bunge la Wawakilishi kuanzia Januari 3.

Hata hivyo huenda azma hiyo ikakumbwa na kigugumiza kutokana na wingi wa wabunge wa chama tawala cha Republican katika Baraza la Seneti.

Maandamano dhidi ya Trump mjini New York

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya utafiti mwingine wa maoni uliofanywa na shirika la habari la CNBC kuonesha kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani anaendelea kupoteza uungaji mkono sio tu miongoni mwa wananchi, bali pia miongoni mwa wafanyabiashara matajiri waliomuunga mkono katika kampeni zake za uchaguzi uliopita mwaka 2016.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 34 tu ya mamilionea nchini Marekani ndiyo wameonesha kuwa watamuunga mkono Trump katika uchaguzi ujao wa rais wa mwaka 2020, ikilinganishwa na asilimia 45 mwaka jana.