Wabunge wenye asili ya Afrika Ufaransa watishiwa kuuawa
Wabunge wenye asili ya Afrika nchini Ufaransa wametumiwa barua zenye vitisho kwamba watauawa huku vitendo vya kuwabagua Waafrika vikiripotiwa kuongezeka katika nchi hiyo ya Ulaya.
Katika tukio la hivi karibuni kabisa, Jean-François Mbaye, ambaye ni mbunge wa chama tawala cha Republic on the Move (REM), amepokea barua ya kibaguzi ambapo, mwandishi ambaye hakueleza jina lake ametishia kumpiga 'risasi kichwani". Mbunge huyo Mfaransa mwenye asili ya Senegal amesema atawasilisha malalamiko rasmi mahakamani kuhusu tishio hilo.
Mbaye amechapisha barua hiyo katika ukurasa wake wa Twitter ambapo mwandishi ameandika kuwa, mbunge hiyo ni miongoni mwa Waafrika wanaotumiwa kuwafanya walimwengu wadhani kuwa Wafaransa si wabaguzi. Mwandishi wa barua hiyo aidha amehoji, "ni vipi Mwafrika anapata haki ya kuingilia matatizo ya Ufaransa'.
Mbaye amesema hashtushwi na ubaguzi huo na kuongeza kuwa, ataendelea kupambana na ubaguzi. Barua hiyo pia imewalenga wabunge wawili wa REM, Laetitia Avia and Hervé Berville. Havia, ambaye wazazi wake ni kutoka Togo, tayari ameshapokea barua yenye matusi ya kibaguzi na tishio la kumuua ambapo waliomwandikia walimtaja kuwa 'nguruwe mnono kutoka Afrika anayeingilia mambo ya ndani ya Ufaransa.
Waziri wa Mazingira Ufaransa François de Rugy, amelaani barua hiyo ya kibaguzi na kutangaza uungaji mkono wake kwa Wabunge hao Waafrika wanaokabiliwa na vitisho vya kuuawa na wabaguzi wa rangi nchini humo.