Trump atishia kutangaza hali ya hatari kushinikiza ujenzi wa ukuta
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50675-trump_atishia_kutangaza_hali_ya_hatari_kushinikiza_ujenzi_wa_ukuta
Huku shughuli za serikali zikiendelea kufungwa kwa wiki ya tatu sasa nchini Marekani, Rais Donald Trump ametishia kuwa ikilazimu atatangaza hali ya hatari ili kushinikiza ujenzi wa ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 06, 2019 03:47 UTC
  • Trump atishia kutangaza hali ya hatari kushinikiza ujenzi wa ukuta

Huku shughuli za serikali zikiendelea kufungwa kwa wiki ya tatu sasa nchini Marekani, Rais Donald Trump ametishia kuwa ikilazimu atatangaza hali ya hatari ili kushinikiza ujenzi wa ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico.

Trump amesisitiza kuwa, yuko tayari kuona baadhi ya shughuli za serikali zinaendelea kufungwa kwa miezi au hata miaka, hadi mvutano kati ya Ikulu ya Marekani (White House) na wanachama wa chama cha Democrats kuhusu ukuta utakapotatuliwa.

Trump amesema shughuli za serikali hazitafunguliwa hadi suala la ujenzi wa ukuta litakapotatuliwa, ujenzi ambao wabunge wa chama cha Democrats wanasema hauna udharura na utawagharimu bure walipa kodi.

Trump na wabunge wa Kongresi katika kikao, Ikulu

Kufungwa kwa shughuli za serikali kwa wiki ya tatu sasa nchini Marekani kumeathiri watu wengi haswa wafanyakazi wa umma laki nane, aghalabu yao wakiwa hata hawajalipwa mishahara ya mwezi uliopita wa Disemba.

Trump anashinikiza kupewa bajeti ya dola bilioni 5.6 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta huo, licha ya kuahidi wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais kuwa ujenzi huo utagharamiwa na serikali ya Mexico.