Wamarekani wamlaumu Trump kwa kufungwa taasisi za serikali ya nchi hiyo
Aghalabu ya wananchi wa Marekani wamesema kuwa Rais Donald Trump ndiye anayepaswa kubebeshwa dhima ya kufungwa kwa taasisi za serikali nchini humo tokeo mwezi uliopita hadi sasa.
Utafiti wa maoni uliofanywa na gazeti la Washington Post kwa kushirikiana na shirika la habari la ABC News umeonesha kuwa, asilimia 53 ya watu waliohojiwa wamesema Trump na chama tawala cha Republican ndio wanaopaswa kulaumiwa kwa kufungwa shughuli za serikali.
Asilimia 29 ya watu walioshirikishwa kwenye utafiti huo wa maoni uliofanywa kati ya Januari 8 na 11 wanaamini kuwa chama cha upinzani cha Democratic ndicho kinapaswa kubebeshwa dhima.
Uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa hivi karibuni kwa pamoja na Redio ya Taifa ya Marekani (NPR) na Taasisi ya Ipsos ulionyesha kuwa, Wamarekani saba kati ya kila ya kumi wanaamini kuwa, kufungwa kwa shughuli za serikali kunaathiri nchi na uchumi na kwamba Kongresi inapaswa kuendelea kufanya mazungumzo na Serikali Kuu ya Marekani kuhusu bajeti ya ujenzi wa ukuta wa mpakani kati ya nchi hiyo na Mexico.
Trump anashinikiza kupewa bajeti ya dola bilioni 5.7 ya ujenzi wa ukuta huo licha ya kuahidi wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais kuwa mradi huo ungesimamiwa na serikali ya Mexico.
Robo ya wafanyakazi wa serikali na watumishi wa Federali 800,000 wameathiriwa moja kwa moja na hatua hiyo ya kufungwa kwa serikali kwa wiki nne sasa.