Kutoshiriki Mogherini katika mkutano wa Warsaw, pigo jingine dhidi ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51039-kutoshiriki_mogherini_katika_mkutano_wa_warsaw_pigo_jingine_dhidi_ya_marekani
Katika fremu ya siasa zake za kuipiga vita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Marekani imeanzisha jitihada kubwa za kuitisha mkutano wa kutafuta mwafaka wa kimataifa dhidi ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 22, 2019 03:41 UTC
  • Federica Mogherini
    Federica Mogherini

Katika fremu ya siasa zake za kuipiga vita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Marekani imeanzisha jitihada kubwa za kuitisha mkutano wa kutafuta mwafaka wa kimataifa dhidi ya Iran.

Imepangwa kuwa mkutano huo utafanyika tarehe 13 na 14 Februari katika mji mkuu wa Poland, Warsaw. Washington inasema kuwa, imezialika nchi 70 katika mkutano huo.

Marekani imeichagua Poland ambaye ni muitifaki wake mkubwa katika eneo la Ulaya mashariki kwa ajili ya mkutano huo hatua ambayo imetambuliwa kuwa ni mbinu ya kutaka kuzusha hitilafu katika Umoja wa Ulaya. Mwaliko huo wa Marekani pia umekataliwa na nchi kubwa wanachama katika Umoja wa Ulaya. 

Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini amethibitisha kuwa, hatashiriki katika mkutano huo wa Marekani dhidi ya Iran uliopewa jina la "Mustakbali wa Mashariki ya Kati". Wiki mbili zilizopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alisema kuwa, mkutano huo wa Warsaw utajikita zaidi katika kukabiliana na miradi ya makombora ya Iran na harakati za nchi hiyo katika eneo la Mashariki ya Kati. Hata hivyo ripoti zilizotolewa katika siku kadhaa zilizopita zimekadhibisha madai ya Marekani iliyosema kuwa, mawaziri wa mambo ya nje wa makumi ya nchi watashiriki katika mkutano huo wa Warsaw na kusema kuwa, nchi nyingi zimetangaza kwamba, hazitashiriki au kwa uchache zitawakilishwa na ujumbe wa ngazi za chini katika mkutano huo. 

Akijibu maswali ya waandishi habari hiyo jana mjini Brussels kabla ya mkutano wa Umoja wa Ulaya, Mkuu wa Sera za kigeni wa Umoja huo, Federica Mogherini alisema: "Nadhani kuwa katika siku za mkutano huo nitakuwa katika mkutano wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa ambao umetayarishwa muda kitambo. Vilevile Nitafanya safari katika eneo la Pembe ya Afrika na kwa msingi huo sidhani kuwa nitakuwa Brussels au hata barani Ulaya kwa ujumla." 

Federeca Mogherini

Japokuwa Mogherini ametaja sababu ya kutoshiriki kwake katika mkutano huo kuwa ni safari yake iliyokuwa tayari imepangwa barani Afrika lakini ni wazi kuwa, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amepuuza mkutano huo wa Marekani na kuutambua kuwa ni kuungana na Washington katika siasa zake za kuipiga vita Iran.

Awali ilikuwa imeripotiwa pia kuwa, Ufaransa yumkini ikatuma ujumbe wa ngazi za chini kabisa katika mkutano wa Warsaw. Ujerumani na Uingereza bado hazijatangaza iwapo zitashiki katika kikao hicho au la. Suala hili linaonesha kuwa, katika jitihada zake za kulinda makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Troika ya Ulaya (Ujerumani, Uingereza na Ufaransa), na Umoja wa Ulaya kwa ujumla zimeamua kutofuata sera hizo zinazoipiga vita Iran.

Marekani daina imekuwa ikishambulia siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu eneo la Mashariki ya Kati na kwa sababu hiyo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo amedai kuwa mkutano huo wa Warsaw ni wa kustawisha amani na uhuru eneo la Mashariki ya Kati.

Pamoja na hayo yote tunapotazama mawaziri wa mambo ya nje waliopangwa kushirki katika mkutano huo tunaona kuwa, ni kutoka nchi zenye fikra na mielekeo inayotofautiana na pengine kupingana ambazo haziwezi kufikia mwafaka juu ya malengo ya Marekani dhidi ya Iran.

Katika mkondo huo huo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Dakta Muhammad Javad Zarif amendika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter akiiambia Poland na washiriki katika mkutano wa Warsaw kwamba: Wale wote walioshiriki katika mkutano uliopita wa Marekani dhidi ya Iran ama wamekufa au wamepoteza heshima na kufedheheka au wametimuliwa; na Iran imekuwa imara na yenye nguvu zaidi kuliko hapo awali."

Zarif na Mogherini

Alaa kulli hal, licha ya madai ya urongo ya Washington ambayo inafanya jitihada za kutaka kudhihirisha ushawishi na nafasi ya Iran katika Mashariki ya Kati kuwa ni jambo baya na hatari, lakini sasa hata waitifaki wa Marekani barani Ulaya wanakiri kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ni nchi muhimu na yenye mchango chanya katika kanda hii. Vilevile hivi sasa na kuliko wakati wowote mwingine, dunia inashuhudia vyema sera za kijuba na kibeberu za Marekani dhidi ya Iran zinazotokana na kuendelea kusimama kidete Tehran kukabiliana na sera za kupenda makuu na kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine za serikali ya Washington.