Naibu Spika wa Ujerumani ataka balozi wa Marekani nchini humo afukuzwe
Naibu Spika wa Bunge la Ujerumani ametoa mwito wa kutimuliwa nchini humo balozi wa Marekani kutokana na kile alichokitaja kuwa uingiliaji wake wa masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Ulaya.
Wolfgang Kubicki, Naibu Spika wa Bunge la Ujerumani amesema serikali ya Berlin inapaswa kutangaza kuwa balozi huyo wa Marekani sio halali kuwa nchini humo na anapaswa kufukuzwa mara moja.
Kubicki amesema, "Subira yetu ina mipaka. Balozi wa Marekani mjini Berlin, Richard Grenell ambaye anajifanya kuwa kamishna wa eneo lililokaliwa kwa mabavu anapaswa kufukuzwa."
Amesema Richard Grenell kwa mara nyingine tena amevuka mpaka, kwa kuingilia siasa za nchi hiyo yenye kujitawala ya kifederali.
Balozi huyo wa Marekani ambaye aliapishwa kuanza majukumu hayo mjini Berlin mwezi Mei mwaka jana ameikosoa Ujerumani kuhusu kupunguza bajeti yake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato).
Marekani na Ujerumani zimekuwa zikisuguana kwa muda sasa. Mwishoni mwa mwaka uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas aliashiria ulazima wa kulindwa na kuhifadhiwa mapatano ya nyuklia na Iran akisisitiza kuwa moja ya njia za kuyalinda mapatano hayo ni kuiweka pembeni Marekani.
Aidha wanasiasa nchini Ujerumani walimjia juu balozi huyo wa Marekani mjini Berlin kwa matamshi yake ya kijuba yaliyo dhidi ya mashirika ya Ujerumani yanayoendesha shughuli zao nchini Iran, wakisisitiza kuwa anapaswa kwenda chuoni kujifunza masuala ya kidiplomasia.