Ubeberu wa Marekani haubakishi mtu, sasa ni zamu ya Italia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ametoa vitisho vipya dhidi ya nchi muitifaki wa Washington yaani Italia kwa kudai kuwa nchi kama Italia ambazo zinataka kujiunga na mradi wa kiuchumi wa China uliopewa jina la "Njia ya Hariri" zitambue kuwa zitapata hasara kubwa ya kisiasa.
Shirika la habari la AFP la nchini Ufaransa limemnukuu Mike Pompeo akitoa vitisho hivyo dhidi ya Italia na kukiri kwamba uamuzi wa nchi mbalimbali wa kufanya miamala ya kibiashara na China umeikatisha tamaa Marekani. Baada ya kuona hawezi kuzifanya chochote nchi hizo, Pompeo amedai kuwa, kushiriki nchi kama Italia katika mradi wa "Njia ya Hariri" wa China ni hasara kwa wananchi wa nchi hizo.
Vile vile amekiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba Marekani haiwezi kushindana na China katika kasi ya ukuaji wa kiuchumi na kuishia kusema kuwa, Washington inatambuwa kwamba ni haki ya China kushiriki katika ushindani wa kibiashara ulimwenguni, lakini inabidi Beijing iwe muwazi katika biashara zake.
Jumamosi iliyopita, Italia ilifikia mapatano ya kuwa mwanachama katika mradi wa China wa "Njia ya Hariri."
Kwa hatua yake hiyo, Italia imekuwa nchi ya kwanza ya kundi lijulikanalo kwa jina la G7 kuwa mwanachama wa mradi huo mkubwa wa China unaoziunganisha nchi nyingi kwa njia za majini na nchi kavu. Sehemu moja ya mradi huo ilifunguliwa mwaka 2013.
Ni kawaida ya Marekani hasa wakati huu wa urais wa Donald Trump kuzifanyia ubeberu nchi zote duniani na kuingilia maamuzi na mambo yao ya ndani bila ya kujali urafiki uliopo baina ya Washington na nchi hizo.