Papa azikosoa nchi zinazojenga ukuta ili kuwafungia nje wahajiri
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewakosoa vikali viongozi wanaojenga ukuta katika mpaka wa nchi zao eti kwa ajili ya kuzuia wimbi la wahajiri.
Papa aliyasema hayo jana Jumapili akiwa njiani kuelekea mjini Rome akitokea Morocco, alipoulizwa kuhusu ujenzi wa ukuta kwa ajili ya kuwazuia wakimbizi na kadhia ya wahajiri kwa ujumla. Bila kutaja kiongozi yeyote moja kwa moja, Papa Francis amesema, "Hao viongozi wa kisiasa wanaojenga ukuta katika mipaka yao wataishia kuwa wafungwa ndani ya kuta walizojenga wenyewe."
Hii ni katika hali ambayo, Rais Donald Trump wa Marekani hivi karibuni alisema kuwa, ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Mexico utaanza ndani ya siku chache zijazo.
Hitilafu zilizojitokeza baina ya Trump na Bunge la nchi hiyo kuhusu uidhinishaji wa bajeti ya ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Mexico, zilisababisha kusimamishwa shughuli za baadhi ya sekta za serikali kuu ya Marekani kuanzia Desemba 22 mwaka jana hadi Ijumaa ya tarehe 25 Januari mwaka huu.
Hali kadhalika Aprili mwaka jana, Utawala wa Kizayuni ulianza tena kujenga ukuta wake wa kibaguzi kati ya mpaka wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Lebanon.
Kabla ya hapo, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianza kujenga ukuta wa zege katika maeneo ya mipaka kati ya Ghaza na Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Tayari utawala huo wa Kizayuni ushajenga ukuta eti wa usalama katika Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan kwa kisingizio cha kuwazuia wanamapambano wa Palestina kuingia katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel na kisha kutwaa mamia ya eka za ardhi za Wapalestina.