Uungaji mkono wa jeshi la Venezuela kwa mpango wa Rais Maduro wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa nchini humo
(last modified Wed, 10 Apr 2019 14:36:26 GMT )
Apr 10, 2019 14:36 UTC
  • Uungaji mkono wa jeshi la Venezuela kwa mpango wa Rais Maduro wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa nchini humo

Mgogoro wa kisiasa nchini Venezuela uliibuka tangu tarehe 10 Januari mwaka huu, wakati Rais Nicolás Maduro wa nchi hiyo aliposhinda kwa kuchaguliwa kwa mara ya pili na kuapishwa kuwa rais wa taifa hilo la Amerika ya Latini, katika uchaguzi ambao ulisusiwa na wapinzani.

Marekani na nchi kadhaa za Ulaya na Amerika ya Latini zilitangaza kumuunga mkono kiongozi wa upinzani Juan Gerardo Guaid, mkabala na nchi nyingi kama vile Russia, China, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Afrika Kusini, Italia, Cuba, Bolivia, Mexico na kadhalika, ambazo sambamba na kulaani hatua hiyo ya Guaido, zilitangaza uungaji mkono wao kwa Nicolás Maduro rais halali wa Venezuela. Kwa kutumia uungaji mkono wa kila upande wa Marekani, Juan Guaidó amekuwa akifanya kila njia ili kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Nicolas Maduro. Aidha Guaidó amekuwa akifanya kila liwezekanalo kuifanya hali ya mambo nchini Venezuela iwe mbaya zaidi ili kwa njia hiyo na kama anavyodhania kwamba baada ya kushtadi mgogoro nchini humo hatimaye ataweza yeye kushika hatamu za utawala. Hata hivyo na licha ya hatua mbalimbali za uharibifu za mpinzani huyo, lakini Rais Nicolás Maduro ametaka yafanyike mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kutatuliwa mgogoro wa kisiasa wa sasa unaoikabili nchi hiyo, suala ambalo limeungwa mkono pia na jeshi la Venezuela. Kuhusiana na suala hilo, Vladimir Padrino López, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo sambamba na kupongeza juhudi za Rais Maduro kwa ajili ya kuimarisha usalama, demokrasia na utamaduni wa mazungumzo, amesema kuwa mashauriano ya pande tofauti katika jamii ni jambo litakalosaidia kudumishwa mfumo wa kiutawala wa nchi hiyo.

Vladimir Padrino López, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela

Aidha Rais Nicolás Maduro amesema, njia za utatuzi zilizopendekezwa katika eneo hilo la Amerika ya Latini kwa ajili ya kutatua mgogoro wa sasa nchini kwake ni zenye taathira chanya amesisitiza kwamba utaratibu uliopendekezwa Montevideo, mji mkuu wa Uruguay, ni wenzo bora wa kutumiwa kwa ajili ya kutatuliwa mgogoro huo. Jumamosi iliyopita, Maduro alizitaka nchi za Mexico, Bolivia, Uruguay na nchi za eneo la Caribbean kuanza kutekeleza kivitendo mpango uliopitishwa miezi miwili iliyopita mjini Montevideo, Uruguay. Mpango wa Montevideo uliobuniwa na Mexico na Uruguay na ambao pia unaungwa mkono wa Bolivia na nchi za ukanda wa Caribbean, ni mpango wenye hatua nne kwa ajili ya kupunguza ongezeko la mizozo kati ya chama tawala cha Kisoshalisti na wapinzani wanaoungwa mkono na Marekani na pia kupatiwa ufumbuzi mizozo hiyo kwa njia za amani kupitia mazungumzo ya pamoja. Katika uwanja huo, Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Jumapili iliyopita alipongeza juhudi za serikali ya Montevideo na kusema kuwa juhudi hizo ni njia stahiki kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro wa kisiasa nchini kwake sambamba na kuiepusha nchi hiyo na mapigano ya silaha. Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter Arreaza alisema kuwa, juhudi hizo ni za dhati zaidi na halisi zaidi katika ubunifu wa kivitendo uliowasilishwa na kwamba siku ya Jumamosi pia Rais Nicolás Maduro alitoa amri ya kutekelezwa kwake.

Rais Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ambaye anazidi kupata uungaji mkono wa wananchi na jeshi 

Kwa mtazamo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, mazungumzo na udiplomasia ni njia ambayo inatakiwa kufuatwa, na kwamba vita na utumiaji mabavu kamwe havina nafasi yoyote nchini Venezuela. Hata hivyo licha ya serikali ya Caracas pamoja na Rais Maduro kuonyesha nia nzuri, lakini wapinzani wao wameendelea kushikilia mpango wa utumiaji nguvu za kijeshi na mabavu wa Washington, wakiamini kwamba njia hiyo ndio inayoweza kuhitimisha mkwamo wa kisiasa, kama ambavyo wanasisitizia kuondolewa madarakani serikali na rais huyo aliyechaguliwa kidemokrasia na wananchi. Aidha katika fremu ya kumuunga mkono Juan Guaidó, Marekani imetekeleza mashinikizo na vikwazo vipya vya kifedha na kiuchumi dhidi ya Venezuela sambamba na kuyawekea vikwazo mashirika ya mafuta ya nchi hiyo. Kama hiyo haitoshi, Washington imefikia hatua ya kutoa vitisho kwa nchi zinazomuunga mkono Rais Nicolás Maduro kama vile Russia na China. Hata hivyo licha ya hatua hizo chafu za Marekani, raia wa Venezuela na bila kuogopa vitisho vya Washington wameendelea kuonyesha uungaji mkono wao kwa Rais Maduro na katika uwanja huo Jumamosi iliyopita makumi ya maelfu ya waungaji mkono kwa serikali ya mrengo wa kushoto ya Caracas walifanya maandamano makubwa na kuonyesha azma yao ya kuendelea kuiunga mkono serikali dhidi ya ubeberu na njama za Washington.

Tags