Guterres akutana na waathiriwa wa shambulizi la kigaidi la New Zealand
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53473-guterres_akutana_na_waathiriwa_wa_shambulizi_la_kigaidi_la_new_zealand
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametadharisha kuwa, matamshi ya chuki na kibaguzi yanaenea kwa kasi ya kutisha mitandaoni, na kusisitiza kuwa UN itaongoza jitihada za kupambana na tatizo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 14, 2019 03:19 UTC
  • Guterres akutana na waathiriwa wa shambulizi la kigaidi la New Zealand

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametadharisha kuwa, matamshi ya chuki na kibaguzi yanaenea kwa kasi ya kutisha mitandaoni, na kusisitiza kuwa UN itaongoza jitihada za kupambana na tatizo hilo.

Antonio Guterres ametoa indhari hiyo leo Jumanne, alipokutana na majeruhi na familia zilizopoteza wapendwa wao katika shambulizi la kigaidi dhidi ya misikiti miwili ya New Zealand mnamo Machi 15 mwaka huu.

Amesema, "Kauli za chuki zinasambaa kama moto wa kichaka kwenye mitandao, lazima tuuzime moto huo. Hakuna nafasi ya kueneza chuki na ubaguzi kwenye mitandao au kwa njia ya moja kwa moja."

Sambamba na kuwafariji waathiriwa wa shambulizi hilo, Katibu Mkuu wa UN amewatakia kila la kheri Waislamu wa mji ulioshambuliwa wa Christchurch, wakati huu wanapotekeleza ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Wahanga wa shambulizi la kigaidi la Christchurch

Weledi wa mambo wanaitakidi kuwa, kampeni ya kueneza chuki dhidi ya Uislamu ndiyo sababu kuu ya kutokea mauaji hayo ya kikatili ya Waislamu zaidi ya 50 walipokuwa wanasali Sala ya Ijumaa katika misikiti miwili ya mjini Christchurch nchini New Zealand mwezi Machi mwaka huu.

Gaidi kwa jina Brenton Tarrant raia wa Australia mwenye chuki dhidi ya Uislamu ambaye alitangaza mwenyewe kuwa mfuasi wa Rais Donald Trump wa Marekani aliyarusha hewani mubashara mauaji hayo ya kinyama aliyoyafanya katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook.