Russia yakosoa vikali chokochoko za jeshi la Marekani dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54258-russia_yakosoa_vikali_chokochoko_za_jeshi_la_marekani_dhidi_ya_iran
Baada ya kujitoa kinyume cha sheria katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani imekuwa ikitekeleza siasa za 'mashinikizo ya juu zaidi' dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 21, 2019 04:48 UTC
  • Russia yakosoa vikali chokochoko za jeshi la Marekani dhidi ya Iran

Baada ya kujitoa kinyume cha sheria katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani imekuwa ikitekeleza siasa za 'mashinikizo ya juu zaidi' dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Utekelezaji wa siasa hizo umepelekea washindani wa Marekani na hata washirika wake wa Ulaya kutahadharisha juu ya hatari ya siasa hizo. Kuhusiana na suala hilo Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kwamba Russia inasikitishwa sana na hatua ya Marekani kuongeza idadi ya wanajeshi wake katika eneo la Asia Magharibi kwa ajili ya kuongeza mvutano na mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema inasikitisha kuona kuwa hakuna hatua zozote zinazchukuliwa kwa lengo la kurekebisha siasa hizo za mvutano za watawala wa White House. Amesema: Marekani inazidisha idadi ya askari wake na kuongeza mashinikizo dhidi ya Iran katika hali ambayo nchi hii katika miaka iliyopita imekuwa ikionyesha subira na kuheshimu ahadi ilizotoa katika fremu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kufikia sasa imekuwa ikifungamana kikamilifu na mapatano hayo.

Sisitizo la Moscow juu ya masuala mawili muhimu, yaani Iran kuheshimu mapatano ya JCPOA licha ya uvunjaji ahadi wa nchi za Ulaya pamoja na njama za Marekani kuvuruga mapatano hayo muhimu ya kimataifa, linaonyesha wazi mkabiliano uliopo kati ya msimamo wa Russia na Marekani kuhusiana na suala zima la siasa zao kuhusu masuala ya Asia Magharibi na hasa eneo nyeti la Ghuba ya Uajemi. Mara kwa mara viongozi wa Moscow wamekuwa wakikosoa siasa haribifu za Marekani katika eneo hili.

Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia

Marekani ambayo siku zote imekuwa ikidai kwamba mashinikizo yake dhidi ya Iran ni ya kisasa na kiuchumi tu, katika siku za hivi karibuni imeongeza maradufu askari jeshi wake katika eneo hili la Ghuba ya Uajemi. Akizungumza Jumatano katika kikao cha Kongresi ya Marekani, Bryan Hook, mjume maalum wa Marekani kuhusiana na masuala ya Iran alidai kwamba: Sisi hatutaki kuishambulia kijeshi Iran lakini pamoja na hayo tutaendelea kutetea maslahi yetu. Msingi wa siasa zetu dhidi ya Iran ni diplomasia ya kisiasa na kiuchumi.

Kabla ya hapo , Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani tarehe 16 Juni pia aliituhumu Iran kuwa ilihusika na mashambulio dhidi ya meli mbili za kubeba mafuta katika Bahari ya Oman na kusisitiza kuendelea kuongeza mashinikizo dhidi ya Iran. Alidai, Marekani haina nia yoyote ya kuanzisha vita na Iran lakini itaendelea kuzidisha mashinikizo ya kidiplomasia na kiuchumi dhidi ya nchi hii.

Marekani inaendesha vita vya kiuchumi dhidi ya watu wa Iran na inasisitiza kudumisha siasa hizo za uhasama. Watawala wa Marekani wamekuwa wakitoa madai ya kutotaka vita na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hali ambayo tayari wameshatuma katika Ghuba ya Uajemi kila aina ya silaha na zana za kivita, zikiwemo mavowari, ndege za kivita aina ya B-52, F15, makombora ya patriot na vikosi vipya ya wanajeshi.

Droni ya kijasusi ya Marekani iliyotunguliwa karibuni na jeshi la Iran

Katika kutoa radiamali yake kuhusiana na uchochezi huo wa kijeshi wa Marekani, Sergei Ryabkov amesema: Kuna hatari kubwa kwa usalama wa eneo hilo (Ghuba ya Ujemi). Kila mtu aliye na nia isiyo ya uwajibikaji  kwa ajili ya kuzidisha mvutano katika eneo, anapaswa kusimamisha mara moja mwenendo huu kabla mambo hayajaharibika.

Nukta nyingine muhimu hapa ni kuwa hata washirika wa Marekani wa Ulaya wanasema kuwa mwenendo huo wa ubabe wa Marekani dhidi ya Iran inavuruga usalama na kuchochea mivutano katika Ghuba ya Uajemi. Ni kwa msingi huo ndipo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani na Ufaransa wakataka kusimamishwa mwenendo huo ili kuzuia mapigano katika eneo. Hivi sasa nchi za Ulaya zina wasiwasi mkubwa kuhusiana na siasa hizo za ubabe wa Marekani katika eneo. Licha ya uchokozi na uchochezi huo wa watawala wa Washington lakini Iran imesisitiza mara nyingi juu ya kulindwa amani na usalama wa eneo nyeti la Ghuba ya Uajemi na kupinga vikali hatua za kuibua machafuko na mvutano za Marekani katika eneo hili. Iran imekuwa ikitumia uwezo wake wote kuhakikisha kuwa amani na utulivu wa kudumu unadumishwa katika eneo.