Kuzidi kuharibika uhusiano wa Marekani na Pakistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57409-kuzidi_kuharibika_uhusiano_wa_marekani_na_pakistan
Siku chache zilizopita, Pakistan haikuruhusu ndege moja ya kijeshi ya Marekani kutumia anga yake ikiwa ni katika kile kinachoonekana ni kuzidi kuharibika uhusiano wa Washington na Islamabad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 21, 2019 23:45 UTC
  • Kuzidi kuharibika uhusiano wa Marekani na Pakistan

Siku chache zilizopita, Pakistan haikuruhusu ndege moja ya kijeshi ya Marekani kutumia anga yake ikiwa ni katika kile kinachoonekana ni kuzidi kuharibika uhusiano wa Washington na Islamabad.

Juzi Jumatano, tarehe 20 Novemba 2019, mtandao wa habari wa ARY News wa Pakistan ulitangaza kuwa, ndege moja ya kijeshi ya Marekani ilitaka kuingia kwenye anga ya Pakistan, lakini kwa vile haikuwa na kibali na rubani hakuwa na code ya kuingilia Pakistan, jeshi la nchi hiyo lilitishia kuitungua, hivyo ndege hiyo ya Marekani ililazimika kurudi nyuma na haikutumia anga ya Pakistan.

Duru za habari zimesema kuwa, Shirika la Ndege la Pakistan limeanzisha uchunguzi kuhusu suala hilo na hadi hivi sasa hakujatolewa ufafanuzi wa kina kuhusu tukio hilo.

Hatua ya Pakistan ya kuizuia ndege ya kivita ya Marekani kutumia anga yake inaonesha kuwa serikali ya Islamabad, tofauti na serikali za huko nyuma za Pakistan, haipendi kuona inaburuzwa na White House na haiko tayari kuiruhusu Marekani kutumia kiholela anga yake bila ya kuomba ruhusa kwanza.

Dola la kkibeberu la Marekani halina mwamana, linajifanya ni rafiki kumbe ni adui yako na linajali maslahi yake binafsi tu

 

Ijapokuwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Pakistan imesema kuwa sababu iliyopelekea kuzuiwa ndege ya kijeshi ya Marekani kutumia anga ya nchi hiyo ni kutokuwa na kibali cha serikali ya Islamabad, lakini jambo hili nalo inadhaniwa lipo kwamba Pakistan hivi sasa haiko tayari tena kuiona Marekani inatumia kiholela anga yake na hairidhishwi na siasa za Washington za kujikumbizia kila kitu upande wake.

Tab'an inabidi tuelewe pia kuwa mzozo katika uhusiano wa Pakistan na Marekani ulianza zamani, tangu mwaka 2004 wakati wa vita vya Afghanistan. Wakati huo Marekani ilitumia ndege zisizo na rubani kufanya mashambulizi katika maeneo ya makabila ndani ya ardhi ya Pakistan. Jambo hilo halikuwafurahisha hata kidogo wananchi wa Pakistan na kwamba vyama mbalimbali vilivyoingia madarakani nchini humo katika kipindi hiki cha miaka 15 iliyopita muda wote vimekuwa na mzozo na Washington kuhusu suala hilo. 

Wakati wa serikali iliyopita ya Pakistan ambapo Waziri Mkuu wa hivi sasa wa nchi hiyo, Imran Khan alikuwa kiongozi wa kundi moja muhimu la kisiasa lililokuwa linaipinga serikali; ukosoaji mkubwa wa Imran Khan wakati huo ulikuwa ni siasa za Marekani katika vita vya Afghanistan na kitendo cha Washington cha kujichukulia maamuzi ya upande mmoja dhidi ya Pakistan kwa madai ya kupambana na makundi ya Taliban na al Qaida. 

Katika miaka ya 2013 hadi 2018, Imran Khan aliongoza maandamano makubwa ya Pakistan nzima ya kuipinga Washington na kulaani mashambulizi ya droni za Marekani kwenye maeneo mbalimbali ya Pakistan tena bila ya idhini ya Islamabad.

Wananchi wa Pakistan katika maandamano ya kulaani uistikbari wa Marekani

 

Hata baadhi ya duru za habari na za kisiasa za Pakistan zinaamini kuwa, moja ya sababu za kupata umaarufu Imran Khan na chama chake kwenye uchaguzi wa bunge wa 2018 ni msimamo wake wa kuipinga Marekani na sisitizo lake la kulindwa kikamilifu heshima na manufaa ya kitaifa ya Pakistan.

Wachambuzi wa mambo wanaamini pia kuwa, Pakistan hivi sasa haina njia nyingine isipokuwa kuchukua hatua mbalimbali za kuonesha kivitendo kwamba haikubaliani na siasa za kibeberu na za upande mmoja wa Marekani hasa kwa kuzingatia kuwa, kilichomuingiza madarakani Waziri Mkuu Imran Khan ni msimamo wake wa kupinga siasa za Marekani za kutoheshimu haki ya kujitawala taifa la Pakistan. 

Jambo jingine linaloonesha kuzidi kuvurugika uhusiano wa Pakistan na Marekani ni tuhuma zinazotolewa na viongozi wa Washington wanaodai kuwa serikali ya Islamabad inaunga mkono ugaidi. Hatua ya Marekani ya kuunga mkono misimamo ya India na Afghanistan dhidi ya Pakistan ni ushahidi mwingine wa kushadidi mzozo kwenye uhusiano wa Washington na Islamabad. Propaganda kubwa zinazoendeshwa na Marekani dhidi ya Pakistan pia zimewakasirisha wananchi na viongozi wa nchi hiyo na kuwafanya wazidi kuchukua msimamo wa kukabiliana na uistikbari wa Marekani. 

Hivyo tunaweza kusema kwa kifua kipana kwamba hatua ya Pakistan ya kuzuia ndege ya kijeshi ya Marekani kutumia anga yake ni muendelezo wa mapambano yanayoendeshwa na Islamabad ya kukabiliana na siasa za kibeberu za Marekani za kujikumbizia kila kitu upande wake.