Trump na madai ya kizandiki ya kuwaunga mkono wananchi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58482-trump_na_madai_ya_kizandiki_ya_kuwaunga_mkono_wananchi_wa_iran
Ijapokuwa tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi mwaka 1979 Marekani siku zote imekuwa ikiamiliana kiuadui na kiuhasama na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini Donald Trump, rais afriti aliyeko madarakani hivi sasa nchini humo, yeye ametia fora na kufurutu mpaka, kwa uadui ambao haujawahi kushuhudiwa, anaoifanyia Iran na wananchi wake.
(last modified 2026-02-15T05:39:07+00:00 )
Jan 13, 2020 07:57 UTC
  • Trump na madai ya kizandiki ya kuwaunga mkono wananchi wa Iran

Ijapokuwa tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi mwaka 1979 Marekani siku zote imekuwa ikiamiliana kiuadui na kiuhasama na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini Donald Trump, rais afriti aliyeko madarakani hivi sasa nchini humo, yeye ametia fora na kufurutu mpaka, kwa uadui ambao haujawahi kushuhudiwa, anaoifanyia Iran na wananchi wake.

Trump

Bila ya soni wala kuwa na chembe ya haya, hivi sasa Trump anadai kuwa, yeye anawaunga mkono wananchi wa Iran. Wakati anawadhikisha Wairani kwa mbinyo wa vikwazo vikali kabisa kupitia sera yake ya "mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa", rais huyo wa Marekani ameandika ujumbe wa kuchekesha kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema, yuko pamoja na wananchi hao. Katika msimamo alioonyesha kufuatia mikusanyiko kadhaa iliyofanyika mjini Tehran kuhusiana na kadhia ya ndege ya Ukraine iliyoanguka hivi karibuni karibu na mji mkuu huo wa Iran, Trump amesema katika ujumbe wake huo wa Twitter ulioandikwa kwa lugha ya Kifarsi: "Mimi tangu mwanzo wa urais wangu, nimesimama pamoja na nyinyi; na serikali yangu itaendelea kukuungeni mkono. Sisi tunayafuatilia kwa makini maandamano yenu ya upinzani na tunapata ilhamu kwa ushujaa wenu."

Marais waliotangulia wa Marekani pia, kuanzia Jimmy Carter na waliomfuatia, wote walikuwa kila mara wakionesha uadui wao kwa Iran kwa namna moja au nyingine. Hatua zao hizo za kiuhasama na kiuadui walizokuwa wakichukua, zimejumuisha uandaaji mazingira ya kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Iran na kuusaidia utawala wa Kibaathi wa Iraq kwa taarifa za kiintelijensia na misaada ya kilojistiki katika vita vya miaka minane dhidi ya Iran, mpaka kufika hadi ya kukabiliana nayo moja kwa moja kijeshi mwishoni mwa vita hivyo, sambamba na kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu kila aina ya vikwazo.

Marais 5 kati ya 6 wa Marekani wa baada ya mwaka 1979, walioifanyia kila aina ya uadui Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kutoka kushoto: Jimmy Carter, George H. W. Bush, Barack Obama, George W. Bush na Bill Clinton 

Pamoja na yote hayo, serikali ya Trump imefuata muelekeo mpya katika kuifanyia uadui Iran, ambao kwa hakika umefikia kiwango cha juu kabisa. Katika hatua ya uvunjaji sheria za kimataifa na ya kigaidi, Trump alitoa amri ya kuuliwa Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) pamoja na aliokuwa ameandamana nao katika msafara wa magari karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq. Bila kujali ubaya na ikrahi ya anachokisema, Trump na maafisa wa serikali yake akiwemo waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo, wamedai kuwa, kamanda Qassem Soleimani alikuwa gaidi, na si shujaa. Hata hivyo kwa jinsi wananchi wa Iran walivyousindikiza na kuuaga mwili wa kamanda huyo na wenzake, walionyesha kuwa hawakushughulishwa na madai hayo ya kifidhuli ya Trump; na wanavyoamini wao, si shahidi Soleimani, bali serikali ya Marekani ndiyo ya kigaidi.

Mamilioni ya Wairani wakiusindikiza na kuuaga mwili wa shahidi Qassem Soleimani

Kwa kuzingatia sisitizo lililotolewa na Iran la kulipiza kisasi kikali kwa Marekani, baada ya mauaji ya kigaidi ya Kamanda Soleimani, Trump alitishia kuwa, atazishambulia sehemu 52 za Iran yakiwemo maeneo ya kiutamaduni na turathi za kihistoria. Kitisho hicho cha Trump kililaaniwa kila pembe ya dunia ikiwa ni pamoja na kukosolewa vilali na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO.

Si hayo tu, lakini kwa kutekeleza sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ili kuilazimisha Iran ikidhi matakwa yake, serikali ya Trump imeiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vikwazo zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia; na kila baada ya muda imekuwa ikiongeza vikwazo vingine vipya kwenye orodha ndefu ya vikwazo vikali ilivyoiwekea Tehran. Hapo awali serikali ya Trump ilikuwa ikidai kwamba, itachunga misingi ya haki za binadamu katika kuiwekea vikwazo Iran, lakini sasa imekiuka bila kificho na kutupilia mbali misingi hiyo. Akiashiria matamshi ya rais wa Marekani aliyezungumzia "vita vya kiuchumi" dhidi ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje Mohammad Javad Zarif amesema: "Mimi ninavipa jina la "ugaidi wa kiuchumi"; kwa sababu vimewalenga raia wa kawaida."

Katika waraka wa utekelezaji iliotoa katikati ya mwezi Desemba 2019 na kuuweka kwenye tovuti yake, wizara ya fedha ya Marekani ilikiri kuwa, moja ya malengo ya vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya sekta ya vyombo vya baharini vya Iran ni kuweka mpaka katika mabadilishano ya  bidhaa za mahitaji ya kibinadamu zinazohitajiwa na Tehran. Hadi kabla ya hatua hiyo , viongozi wa Marekani walidai kuwa, bidhaa za vyakula na dawa hazitajumuishwa kwenye vikwazo. Lakini hivi sasa viongozi wa Washington wameamua kutupilia mbali hata matamshi yao hayo ya kujitoa kimasomaso na kusisitiza waziwazi kuwa, watashadidisha mashinikizo dhidi ya wananchi wa Iran kwa kuwawekea vizuizi katika kujidhaminia bidhaa za vyakula na dawa.

Moja ya hatua ya wazi ya kinyama na isiyo ya ubinadamu ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni kuweka vizuizi makusudi vya kuwazuia Wairani wasipate dawa muhimu na za dharura, hususan za wagonjwa wenye maradhi maalumu kiuthakili. Kwa mujibu wa tovuti ya stesheni ya redio ya SRF ya Uswisi, ili kuiwekea mbinyo Iran, Marekani imeiwekea vikwazo Tehran pamoja na nchi na pande zote zinazoshirikiana nayo kibiashara; lakini hatua hiyo imesababisha uhaba wa bidhaa za dawa na chakula nchini Iran na kuhatarisha maisha ya watu wengi hasa wagonjwa wa saratani.

Wagonjwa wa saratani wanaoatilika kwa kukosa dawa kutokana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Kutokuwa na tija vikwazo vya kinyama na visivyo na ubinadamu vya Washington, ambavyo lengo lake ni kuipigisha magoti Tehran ikubali matakwa yake haramu na ya kibeberu, vimeifanya serikali ya Trump iamue kuweka kando vizoro vyote vya kizandiki na kimaonyesho katika kuifanyia uadui na kuiwekea mashinikizo Iran na kushadidisha dhahiri shahiri hatua zake za kinyama dhidi ya wananchi wa Iran.

Katika hali na mazingira kama haya, inashangaza kumuona Trump akikurupuka na kudai kwa mara nyingine kwamba, anawaunga mkono wananchi wa Iran; ilhali yeye mwenyewe ndiye msababishaji halisi wa mlolongo wa matukio yaliyopelekea hatimaye kuanguka ndege ya abiria ya Ukraine.../