EU yapinga njama za Trump dhidi ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58953-eu_yapinga_njama_za_trump_dhidi_ya_wapalestina
Umoja wa Ulaya umepinga mpango uliopendekezwa na Rais Donald Trump wa Marekani ambao unakandamiza haki za taifa la Palestina uliopewa jina la "Muamala wa Karne" ukisisitiza kuwa, mpango huo unakanyaga sheria za kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2020 01:16 UTC
  • EU yapinga njama za Trump dhidi ya Wapalestina

Umoja wa Ulaya umepinga mpango uliopendekezwa na Rais Donald Trump wa Marekani ambao unakandamiza haki za taifa la Palestina uliopewa jina la "Muamala wa Karne" ukisisitiza kuwa, mpango huo unakanyaga sheria za kimataifa.

Hayo yalisemwa jana Jumanne na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya akiwa mjini Brussels alikorejea baada ya kumaliza safari yake ya Asia Magharibi ambapo alizitembelea Jordan na Iran.

Amesema mpango huo wa Marekani uliozinduliwa Januari 28, namna ulivyo hivi sasa unakengeuka vigezo vinavyokubalika vya kimataifa.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa EU ameeleza bayana katika taarifa hiyo kuwa, "ili kupatikana haki na amani ya kudumu, masuala yenye utata yanapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo yatakayozijumuisha pande mbili husika. Hatua za kuendelea kuporwa ardhi na ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Wapalestina haziwezi kupita bila kupingwa."

Amesema serikali za nchi za Ulaya zingali zimeshikilia msimamo wao wa kupinga ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Miinuko ya Golan ya Syria, tangu ardhi hizo zighusubiwe na kukaliwa kwa mabavu na Israel mwaka 1967.

Vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina

EU imetoa taarifa hiyo katika hali ambayo, hivi karibuni Umoja wa Mataifa pia ulisema bado unafungamana na maazimio ya Baraza la Usalama la umoja huo kuhusiana na mji wa Quds na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa vipengee vya mpango huo wa Kimarekani-Kizayuni, mji wa Quds utakabidhiwa kwa utawala khabithi wa Israel, wakimbizi wa Kipalestina wanaoishi nchi tofauti za dunia hawatoruhusiwa kurejea katika ardhi zao za asili, huku taifa la Palestina likisalia tu na ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.