Vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Rusia na Belarus
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64006-vikwazo_vya_umoja_wa_ulaya_dhidi_ya_rusia_na_belarus
Ikiwa ni muendelezo wa uingiliaji wa nchi za Magharibi wa masuala ya ndani ya mataifa mengine, sasa hivi Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kutekeleza kivitendo vikwazo dhidi ya Russia na Belarus.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2020 03:00 UTC
  • Vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Rusia na Belarus

Ikiwa ni muendelezo wa uingiliaji wa nchi za Magharibi wa masuala ya ndani ya mataifa mengine, sasa hivi Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kutekeleza kivitendo vikwazo dhidi ya Russia na Belarus.

Kisingizio kilichotumiwa kuhusu vikwazo hivyo ni madai kwamba Russia ilimpa sumu mpinzani wa serikali ya Moscow, Alexei Navalny. Amma kuhusu Belarus, Umoja wa Ulaya umetumia madai ya uchaguzi wa rais na kushinda Rais Alexander Lukashenko katika uchaguzi huo, kuiwekea vikwazo.

Umoja wa Ulaya (EU) unadai umeiwekea vikwazo Belarus ili kuonesha kuwa umoja huo uko pamoja na wananchi wa nchi hiyo. Machafuko yalianza nchini Belarus tarehe 9 mwezi huu wa Oktoba baada ya Rais Alexander Lukashenko kutangazwa mshindi. Hata hivyo Lukashenko anasema kuwa machafuko hayo yanachochewa na nchi za Magharibi ambazo hazilipendei kheri taifa la Belarus.

Alexei Navalny

 

Tukija katika madai kwamba Russia imempa sumu mpinzani wa serikali ya Moscow, Alexei Navalny, madai hayo yametolewa na EU hususan Ujerumani katika hali ambayo Kremlin imeyapinga vikali ikizitaka nchi za Magharibi zitoe ushahidi, na hadi hivi sasa hazijatoa.

Kwa kweli siasa za vikwazo ni tabia ya muda mrefu ya nchi za Magharibi na Marekani kwa shabaha ya kufanikisha malengo yao haramu kama vile kuingilia masuala ya ndani ya nchi husika. Sasa hivi wataalamu wa mambo wanasema kuwa, Ujerumani imeng'ang'ania suala la kupewa sumu na Russia, Alexei Nafalny ili kuiweka chini ya mashinikizo zaidi Moscow na kujaribu kufanikisha malengo yake kupitia mradi wa bomba la gesi lijulikanalo kwa jina la Nord Stream 2.

Matamshi makali yaliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumaini, Heiko Maas kwamba huenda Ujerumani ikaangalia upya uungaji mkono wake kwa mradi wa bomba la gesi la Nord Stream 2 kama Russia haitaonesha ushirikiano unaotakiwa kuhusu kupewa sumu kiongozi wa wapinzani wa nchi hiyo, ni ushahidi tosha wa ukweli huo.

Norbert Röttgen, Mkuu w Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ujerumani amesema: Ujerumani itaingia katika hatari ya kuwa tegemezi kwa Russia iwapo itaendelea kuunga mkono mradi wa bomba la gesi la kilomita 1225 la Nord Stream.

Mradi wa bomba la gesi la  Nord Stream 2

 

Hatua ya Umoja wa Ulaya ya kutangaza vikwazo dhidi ya Russia kwa kweli ni aina fulani ya siasa za kindumilakuwili za umoja huo. Kwa upande mmoja, viongozi wa EU wanasisitiza kufuata siasa zilizo nyepesi na zinazonyambulika kutokana na umuhimu wa kijiografia wa Russia, kupakana kwake na nchi za Ulaya na utajiri mkubwa wa gesi wa nchi hiyo. Hayo yalisemwa na viongozi hao wa Ulaya masaa machache tu baada ya kutangaza vikwazo dhidi ya Russia. Viongozi wa EU walisema, wana hamu ya kuishi kwa usalama na amani na jirani yao Russia na kuwa na uhusiano mzuri wa kiuchumi. Hata Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani alisema muda mchache baada ya kuwekwa vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya kwamba licha ya kuweko kadhia ya Navalny, lakini Ujerumani ina hamu ya kulinda uhusiano mzuri au kwa uchache wa kimantiki baina yake na Russia. Lakini katika upande mwingine, siasa za EU sasa hivi ni za kupiga ngoma ya vikwazo na kuongeza mashinikizo dhidi ya Russia. 

Amma kuhusu Belarus, Umoja wa Ulaya unatumia pia siasa za kindumilakuwili kama inavyofanya Marekani. Lengo la nchi za Magharibi ni kumng'oa madarakani Rais Alexander Lukashenko wa nchi hiyo ya Ulaya Mashariki. Wamagharibi wanataka watu wenye mielekeo ya Magharibi na maadui wa Russia ndio watawale huko Belarus. Hata hivyo nchi hiyo iliuonya mapema Umoja wa Ulaya kwamba vikwazo vyake dhidi ya Belarus vinaweza kuwa na matokeo usiyoyatarajia kama vile kujitoa Belarus katika miradi ya pamoja na kuangalia upya kiwango na aina ya uhusiano wake na nchi za Ulaya kulingana na maslahi yake ya kitaifa. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, mbali na kwamba uzoefu unaonesha kuwa, siasa za vikwazo dhidi ya mataifa mengine huwa hazizai matunda yaliyotarajiwa, lakini pia kuendelea vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia na Belarus, hakuna faida kwa yeyote zaidi ya madhara tu hasa kwa watu wa kawaida wasio na hatia.