Serikali ya Ufaransa yafunga baadhi ya misikiti nchini humo
Serikali ya Ufaransa imeamua kufunga baadhi ya misikiti nchini humo ikiwa ni katika hatua zake dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu na Waislamu.
Gerald Darmanin Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa ametangaza kufunga misikiti, shule binafasi na maduka 73 kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020. Viongozi wa serikali ya Ufaransa katika miezi ya karibuni wameshadidisha siasa na hatua zao za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa amebainisha hayo ambapo siku kadhaa zilizopita Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo pia alitoa hotuba dhidi ya Uislamu aliposema kwamba Uislamu upo katika mgogoro ulimwenguni kote. Katika mwendelezo wa sera za kupiga vita Uislamu nchini Ufaransa, Emmanuel Macron mwezi uliopita alizindua mpango wa kulinda thamani za kisekulari za nchi hiyo dhidi ya kile kilichotajwa kuwa "misimamo mikali ya Kiislamu."
Katika hotuba yake hiyo ambayo imewaudhi Waislamu wa Ufaransa, Macron alisema, serikali yake itawasilisha muswada mwezi Desemba wa kuimarisha sheria ya 1905 ya nchi hiyo ambayo ilitenganisha rasmi Kanisa na utawala.
Viongozi wa Ufaransa wanatoa madai hayo dhidi ya Uislamu katika hali ambayo serikali za Ulaya ikiwemo ya Ufaransa zilikuwa waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi huko Iraq na Syria.