Malalamiko ya wanawake dhidi ya Trump na mustakbali wa rais huyo wa Marekani
(last modified Mon, 19 Oct 2020 06:17:44 GMT )
Oct 19, 2020 06:17 UTC
  • Malalamiko ya wanawake dhidi ya Trump na mustakbali wa rais huyo wa Marekani

Katika siku zilizopita, wanawake nchini Marekani walifanya maandamano katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo likiwemo la Washington ili kutangaza upinzani wao kwa siasa za rais wa nchi hiyo, Donald Trump. Shabaha ya maandamano hayo ilikuwa ni kupinga ubaguzi wa rangi na ukandamizaji dhidi ya wanawake. Waendeshaji wa maandamano hayo waliahidi kuendelea na operesheni hiyo waliyoipa jina la maandamano 429 katika mikoa 50 ya Marekani.

Wanawake hao wa Marekani wanasema kukwa, zaidi ya wanawake laki moja na 16 elfu wameahidi kushiriki katika maandamano hayo siku zijazo.

Harakati ya wanawake wa Marekani iliundwa mwaka 2017 baada ya Donald Trump kutangazwa rais wa nchi hiyio. Harakati hiyo inafanya maandamano mwezi wa Januari kila mwaka. Hata hivyo hivi sasa hii ni mara ya pili kuandaliwa maandamano hayo kwa mwaka huu wa 2020. Maandamano ya sasa hivi yameitishwa baada ya kufariki dunia jaji wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo, Bi. Ruth Bader Ginsburg na Donald Trump kumteua Amy Coney Barrett kushika nafasi hiyo.

Siasa na misimamo ya Donald Trump katika miaka ya hivi karibuni imechochea sana hasira za wanawake nchini Marekani. Miongoni mwa hatua za Trump zilizowakasirisha wanawake huko Marekani ni misimamo yake katika masuala ya afya na matibabu, mazingira, masuala ya wahajiri, ubaguzi wa rangi, ukandamizaji na kutojali haki za wanawake.

Rais wa Marekani, Donald Trump

 

Katika upande wa afya na matibabu pia hali ni hivyo hivyo. Msimamo wa Trump  katika suala la kuavya mimba, kuondoa sehemu kubwa ya ruzuku iliyokuwa inawasaidia wananchi wa Marekani katika bima hususan baada ya nchi hiyo kughariki kwenye dimwi la ugonjwa wa COVID-19 na bei ya dawa na matibabu kupanda vibaya, ni katika mambo mengine yaliyowakasirisha sana wanawake wa Marekani. Hatua ya Trump ya kudharau ugonjwa wa corona na kulazimisha shule nyingi kufunguliwa bila ya kujali maonyo ya watu wa afya na ughali wa dawa na matibabu kumepelekea idadi kubwa ya wananchi wa Marekani kuwa wahanga wa COVID-19 suala ambalo limewachukiza wanawake wengi wa nchi hiyo.

Kutojali Trump suala la mazingira na kujitoa kwake katika makubaliano ya Paris ya mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kudharau kwake sheria za kulinda mazingira ni mambo mengine yaliyowakasirisha sana wanawake wa Marekani na kuamua kuitisha maandamano ya kulalamikia siasa mbovu na za kibaguzi za rais wa nchi hiyo, Donald Trump. 

Jambo jingine lililowakasirisha mno wanawake nchini Marekani ni kuongezeka ukandamizaji, machafuko na ubaguzi wa rangi kunakochochewa na serikali ya Trump. Ijapokuwa ubaguzi wa rangi umekita mizizi katika historia ya Marekani lakini umeongezeka kupindukia katika kipindi cha tangu kuingia madarakani Donald Trump. Kuuliwa kiholela Wamarekani wasio wazungu kunakofanywa hasa na jeshi la polisi ma kukosekana uadilifu katika ugawaji wa nafasi za masomo na ajira kumeongezeka sana wakati wa utawala wa Trump na kumewakasirisha mno wanawake wa nchi hiyo. Takwimu zinaoenesha kuwa, ukosefu wa ajira kati ya wanawake wa jamii za wachache waishio Marekani umefikia kiwango cha juu sana hivi sasa hata kabla ya wimbi la ugonjwa wa COVID-19 na sasa kiwango hicho kimekuwa maradufu zaidi ya ilivyokuwa kabla ya corona.

Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi

 

Sheryl Sandberg mwandishi maarufu na mkuu wa kitengo cha utendaji cha mtandao wa kijamii wa Facebook ameandika: Hatupaswi kupoteza hata sekunde moja katika jitihada za kutatua matatizo ya kimfumo waliyo nayo wanawake nchini Marekani. Zaidi ya thuluthi moja ya wanawake wamepoteza ajira zao kutokana na corona na wengine wamepewa likizo ya lazima au kupunguziwa mishahara yao. Hali ya wanawake wasio wazungu ni mbaya sana huku wanawake wenye asili ya Afrika wakidhuriwa maradufu na hali hiyo ikilinganishwa na wanaume wazungu.

Kiujumla ni kwamba uamuzi wa wanawake wa Marekani wa kuendeleza maandamano ya kumpinga Donald Trump umeitia kiwewe timu ya kampeni ya rais huyo huku zikiwa zimebakia chini ya siku 20 hadi kufanyika uchaguzi wa rais wa tarehe 3 Novemba huko Marekani. Hasa kwa kuzingatia kwamba, uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa, mpinzani wa Trump yaani Joe Biden anaendelea kumpiku Donald Trump. Aidha uchunguzi wa uchaguzi za rais wa Marekani katika kipindi cha miaka 70 iliyopita unaonesha kuwa, Biden hivi sasa ana uungaji mkono mkubwa mno wa wanawake wapiga kura ambao hajawahi kuupata mgombea yoyote mwingine katika chaguzi zote za miaka 70 iliyopita huko Marekani.

Tags