Taathira za vikwazo vya Marekani kwa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF)
(last modified 2020-10-22T12:52:26+00:00 )
Oct 22, 2020 12:52 UTC
  • Taathira za vikwazo vya Marekani kwa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF)

Gavana wa Benki Kuu ya Iran amesema kuwa, Mfuko wa Fedha Kimataifa (IMF) unapaswa kujibu ombi la Iran la kupewa mkopo kutoka kwenye bajeti ya dharura ya IMF kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya corona, na usikubali kuathiiwa na lobi za kisiasa na mashinikizo ya Marekani.

Abdolnaser Hemmati  alisema jana kuwa Iran imechukua hatua zinazofaa za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona kwa kutumia vyanzo vyake na kuongeza kuwa: Hata hivyo vikwazo visivyo vya kisheria vya Marekani vinaizuia Jamhuri ya Kiislamu kuingiza nchini fedha zake zilizoko nje ya nchi.

Baada ya kuanza maambukizi ya corona, Iran iliomba mkopo kutoka Mfuko wa Fedha wa Kimataifa lakini Marekani ilipinga suala hilo na hatimaye jina la Iran liliondolewa kwenye orodha ya nchi zilizoomba mkopo ya taasisi hiyo. Hali imeendelea hivyo hata baada ya kupita zaidi ya miezi 8 tangu kuliporipotiwa mlipuko wa corona mwishoni mwa mwaka uliopita. 

Sambamba na mlipuko huo mkubwa wa janga la corona, Marekani imezidisha vikwazo vya uchumi dhidi ya taifa la Iran na imeenda mbali zaidi kwa kuzuia hata kuingizwa nchini fedha za kigeni za Iran zilizoko nje ya nchi. Mwenendo huo wa Marekani ni sehemu ya siasa haribifu za serikali ya Washington ambazo zinalenga moja kwa moja maisha na uhai wa wananchi wa kawaida wa Iran; na hapana shaka kuwa suala hili linakiuka sheria na kanuni za kimataifa.

Hii ni katika hali ambayo walimwengu wana matarajio kwamba taasisi muhimu za kimataifa zinapaswa kutekeleza vyema majukumu yao hususan katika kipindi nyeti cha sasa cha mapambano dhidi ya virusi vya corona, na kwamba siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani zinachafua na kuharibu hadhi na utendaji wa taasisi hizo hususan IMF. 

Mfuko wa Fedha wa Kimataifa una majukumu matatu muhimu. Kwanza ni kufuatilia mabadilishano na miamala ya kifedha na kiuchumi ya nchi 189 wanachama, pili ni kutoa ushauri kwa nchi hizo, na tatu ni kutoa mikopo ya muda mfupi na kuzisaidia nchi zinazosumbuliwa na matatizo ya kifedha. Katika kipindi cha sasa ambapo virusi vya corona vinaendelea kuzisumbua nchi mbalimbali duniani, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano wa pande zote na misaada ya kifedha kwa ajili ya kufanikisha mapambano ya kukabiliana na janga hilo lisilo na mpaka; na vikwazo havipaswi kukwamisha shughuli za kibiashara na masuala ya kibinadamu.

Mapambano dhidi ya virusi vya corona yamezidisha bajeti ya nchi mbalimbali mbazo zinahitajia fedha zaidi kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo hatari; na hapa ndipo kazi ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ya kutoa mkopo kwa nchi wanachama inapopata maana yake halisi. 
Inatupasa kusema kuwa, licha ya IMF kuathiriwa na mashinikizo ya kisiasa na vikwazo vya Marekani, jamii ya wanasayansi na makampuni ya Iran yamefanikiwa kuzalisha vifaa vya kukabiliana na maambukizi ya corona ikiwa ni pamoja na aina mbalimbali za vifaa maalumu vya kupima corona (test kit) na mashine za kusaidia wagonjwa wa COVID-19 kupumua (ventilator). 

Iran ambayo ni miongoni mwa nchi waasisi wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa, inashirikiana ipasavyo na jamii ya kimataifa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya corona na hapana shaka kuwa misaada na ushirikiano wa mfuko huo vinaweza kuboresha zaidi na kuimarisha mapambano hayo. 

Kama alivyosema Gavana wa Benki Kuu ya Iran akimwambia Mkuu wa IMF: Virusi vya corona mi mgogoro wa dunia nzima unaohitajia zaidi ushirikiano wa kimataifa kuliko wakati mwingine wowote; na hakuna nchi itakayosalimika na janga hilo peke yake bila ya kupatikana suluhisho la kimataifa la corona.          

Tags