Rais wa Indonesia akosoa undumakuwili wa Wamagharibi kuhusu uhuru wa kujieleza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64369-rais_wa_indonesia_akosoa_undumakuwili_wa_wamagharibi_kuhusu_uhuru_wa_kujieleza
Rais Joko Widodo wa Indonesia amekosoa undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusu uhuru wa maoni na kujieleza na kusema: "Uhuru wa maoni ambao unavunjia heshima matukufu ya kidini haukubaliki."
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 01, 2020 11:49 UTC
  • Rais wa Indonesia akosoa undumakuwili wa Wamagharibi kuhusu uhuru wa kujieleza

Rais Joko Widodo wa Indonesia amekosoa undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusu uhuru wa maoni na kujieleza na kusema: "Uhuru wa maoni ambao unavunjia heshima matukufu ya kidini haukubaliki."

Rais wa Indonesia pia amelaani kauli ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa dhidi ya Uislamu na kusema mtawala huyo amewatusi Waislamu wote duniani.

Ameongeza kuwa kauli ya Macron inaweza kuibua migonga baina ya wafuasi wa dini mbali mbali duniani katika kipindi hiki ambacho dunia inahitaji umoja ili kukabiliana na janga la COVID-19.

“Uhuru wa maoni haupaswi kutumiwa kwa njia ambayo inavunjia heshima matukufu ya kidini,” aliongeza Rais wa Indonesia katika mkutano na waandishi habari kwa njia ya intaneti.

Halikadhalika amelaani vikali hujuma za kigaidi ambazo zilijiri Paris na Niece Ufaransa na kusema Indonesia inatoa wito wa umoja na kustahamiliana kidini kwa ajili ya kujenga dunia bora.

Rais wa Indonesia amebainisha masikitiko yake kuwa Macron amenasibisha hujuma za kigaidi na Uislamu na kusema hilo ni kosa kubwa. “Ugaidi ni ugaidi. Magaidi ni magaidi. Ugaidi hauna uhusiano wowote na dini yoyote ile,” ameongeza.

Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia imetangaza kuwa balozi wa Ufaransa nchini humo ametahadahrishwa kuhusu kitendo cha Macron cha kuuvunjia heshima Uislamu.

Rais Macron wa Ufaransa anaendelea kukosolewa na Waislamu kimataifa kutokana na matamshi yake ya kuutusi Uislamu na Mtume Muhammad SAW. Matamshi hayo yameibua maandamano ya kumlaani huku kukianzishwa kampeni ya kutaka bidhaa zote za Ufaransa zisusiwe.