HRW: Imarati imetuma mamia ya vijana wa Kisudan kupigana vita Libya
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lenye makao yake makuu mjini New York nchini Marekani limetangaza kuwa, kampuni ya huduma za ulinzi na usalama ya Black Shield ya Imarati iliajiri karibu vijana 270 za Kisudani kwa ajili ya kufanya kazi za ulinzi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) lakini vijana hao walijikuta wakitumwa Libya kwenda kupigana katika safu za jenerali muasi, Khalifa Haftar.
Ushahidi uliotolewa na baadhi ya vijana hao unasema kuwa, baada tu ya kuwasili Abu Dhabi huko Imarati Septemba mwaka jana, vijana hao walipokonywa pasi zao za kusafiria na simu za mkononi na wakaanza kupewa mafunzo ya kijeshi. Baadaye walisafirishwa kwa ndege na kupelekwa katika kambi ya kijeshi ya Ras Lanuf inayodhibitiwa na wapiganaji wa Haftar huko Libya bila ya wao wenyewe kujua wanapelekwa wapi.
Vijana hao wanasema walidanganywa na kampuni hiyo ya Imarati na kujikuta katika vita vya ndani vya Libya.
Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa serikali ya Imarati imekataa kujibu au kutoa maelezo yoyote kuhusiana na kashfa hiyo.
Mwezi Julai mwaka huu maelfu ya Wasudani waliandamana hadi mbele ya ubalozi wa Imarati mjini Khartoum kulalamikia kitendo cha serikali ya nchi hiyo cha kuwahadaa na kuwapeleka vitani nchini Libya mamia ya vijana wa nchi hiyo badala ya kuwapeleka Imarati kwa ajili ya kazi.
Ripoti rasmi zinasema kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati unakodi mamluki kutoka nchi za Afrika na kuwapeleka Libya ili wakalisaidie kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na jenerali muasi, Khalifa Haftar.
Katika ripoti yake ya mwezi Desemba 2019, Umoja wa Mataifa ulithibitisha kuwepo wapiganaji wa Sudan katika vita vya Libya ambako wanapigana bega kwa bega na wapiganaji wa Khalifa Haftar anayeungwa mkono na kusaidiwa na Imarati.