Juhudi za Ufaransa za kujaribu kupunguza hasira ya Waislamu duniani
Uadui wa viongozi wa Ufaransa dhidi ya Uislamu, umeamsha hasira ya Waislamu katika pembe zote za dunia kadiri kwamba nchi nyingi za Kiislamu zimelaani msimamo huo wa Wafaransa, bali zimeanzisha harakati za kususia bidhaa zinazotengenezwa Ufaransa ili kuonyesha kuchukizwa kwao na uadui huo wa viongozi wa Paris.
Hasira na radiamali hiyo ya Waislamu si tu kwamba imewalazimu viongozi wa nchi hiyo ya Magharibi kujaribu kuficha chuki waliyonayo dhidi ya Uislamu bali wanafanya jitihada za kuwapoza Waislamu kama inavyodhihiri katika matamshi ya karibuni ya Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa aliyesema: Sisi tunauheshimu sana Uislamu.
Jean-Yves Le Drian ambaye amefanya safari nchini Misri kwa lengo la kuwatuliza Waislamu kutokana na hatua ya rais wa Ufaransa ya kuuunga mkono wazi wazi hatua ya kuchapishwa vikatuni vinavyomshalilisha Mtume Mtukufu (saw) amedai mbele ya viongozi wa nchi hiyo ya Kiarabu kwamba anauheshimu sana Uislamu na kwamba kile wanachopigana nacho wao ni ugaidi ambao umeteka na kutumia vibaya dini.
Jean-Yves Le Drian amefanya safari huko Misri katika hali ambayo katika wiki chache zilizopita hatua ya jarida la Charlie Hebdo linalochapishwa Ufaransa ya kuchapisha vikatuni vinavyomvunjia heshima Mtume Mtukufu (saw) na kisha kitendo hicho kinachouhujumu Uislamu kuungwa mkono na Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa kisingizio cha kutete uhuru wa kusema na kujieleza, imeamsha hasira kali ya Waislamu kote duniani. Kwa kadiri kwamba katika nchi nyingi za Kiislamu bendera ya Ufaransa pamoja na picha za Macron zimechomwa moto na maandamano makubwa kufanyika katika balozi za nchi hiyo ambapo Waislamu wamewataka viongozi wa Ufaransa wawaombe radhi Waislamu.
Wakati huo huo, bidhaa za Ufaransa zimesusiwa katika nchi nyingi za Waislamu.
Katika uwanja huo, baadhi ya wasomi wa Ufaransa wanasema kuwa Emmanuel Macron alifanya kosa kubwa na la wazi dhidi ya Uislamu ambapo sasa madhara yake yamewapata watu wasio na hatia. wanasema, matamshi ya Macron yameleta hasara kubwa kwa bidhaa zinazotengenezwa Ufaransa kwa sababu baadhi ya watu sasa wanasusia bidhaa hizo.
Katika wiki chache zilizopita, rais wa Ufaransa amekuwa akitetea uvunjiwaji heshima matukufu ya dini ya Uslamu kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kijieleza na kudai kwamba kuna uhuru mkubwa nchini humo.
Hii ni katika hali ambayo kundi moja la wasomi na wanafikra wa kimataifa wametoa taarifa wakiwahutubu watu wote duniani na hasa Wafaransa na kusisitiza kuwa demokrasia haiwezi kutekelezwa kwa kubaguliwa kundi moja la jamii na kupendelewa jingine.
Taarifa hiyo inasema kuwa Ufaransa yenyewe ina sheria ambazo zinasisitiza udharura wa kuheshimiwa haki za binadamu zikiwemo za kupambana na ubaguzi wa rangi na kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini lakini kwa bahati mbaya zinapuuzwa na viongozi wa nchi hiyo kwa sababu ya malengo ya kisiasa.
Nchi za Kiislamu zimekuwa zikiwakosoa sana viongozi wa Ufaransa kutokana na msimamo wao wa chuki dhidi ya Uislamu. Kwa mtazamo wa Waislamu, msimamo kama huo unatoa mwanya kwa makundi ya kigaidi na kitakfiri kutumia vibaya Uislamu na hivyo kufanya hali ya Waislamu wanaoishi katika nchi za Magharibi kuwa ngumu zaidi.
Ni kwa kutambua ukweli huo na kwa ajili ya kutetea maslahi yao ya kiuchumi ndipo viongozi wa Ufaransa wakachukua hatua ya kujaribu kupunguza hasira ya Waslamu ambao wametusiwa wazi wazi matukufu yao. Wafaransa wanahofia kupoteza maslahi yao ya kiuchumi katika nchi za Kiislamu tena katika mazingira haya magumu ya kuenea virusi vya corona duniani.
Licha ya juhudi zinazofanywa na viongozi wa Paris katika uwanja huo lakini ni wazi kuwa msimao uliochukuliwa na viongozi wa Ufaransa dhidi ya matukufu yao si jambo linaloweza kusamehewa wala kusahaulika kirahisi.