Kikao cha kimataifa cha London cha kupambana na Ufisadi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i7003-kikao_cha_kimataifa_cha_london_cha_kupambana_na_ufisadi
Kikao cha kimataifa cha kupambana na ufisadi kilimalizika jana usiku mjini London, Uingereza. Viongozi wa kisiasa na kiuchumi waliohudhuria kikao hicho wamesisitiza juu ya kuandaliwa ramani ya njia ya kivitendo kwa ajili ya kupambana na ufisadi wa fedha na ukwepaji kodi ambao unaandaa mazingira ya vitendo vya ukatili ulioratibiwa, ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 13, 2016 12:00 UTC
  • Kikao cha kimataifa cha London cha kupambana na Ufisadi

Kikao cha kimataifa cha kupambana na ufisadi kilimalizika jana usiku mjini London, Uingereza. Viongozi wa kisiasa na kiuchumi waliohudhuria kikao hicho wamesisitiza juu ya kuandaliwa ramani ya njia ya kivitendo kwa ajili ya kupambana na ufisadi wa fedha na ukwepaji kodi ambao unaandaa mazingira ya vitendo vya ukatili ulioratibiwa, ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka.

Katika kikao hicho, nchi sita washiriki ikiwemo mwenyeji Uingereza, Afghanistan na Nigeria zimekubaliana kuyafichua na kuyatangaza hadharani majina ya wamiliki halisi wa mashirika yote yanayofanya shughuli zao katika nchi hizo. Imeelezwa kwamba kufichwa majina ya wamiliki halisi wa mashirika hayo ni moja ya sababu kuu za kushamiri ufisadi wa fedha. Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan alisema katika kikao hicho kwamba mahitaji ya madawa ya kulevya katika masoko ya nchi za Magharibi ndio sababu kuu ya kukithiri ufisadi katika nchi yake. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, yeye alisema, mzunguko wa fedha haramu, thamani yake inakadiriwa kufikia dola trilioni 1.62 na kuongeza kwamba, kiwango hicho ni sawa na kujumuisha pamoja uchumi wa Afrika Kusini, Ubelgiji na Uswisi. Cameron ameeleza kwamba lengo la kuitishwa kikao hicho ni kufanya jitihada za kuutangaza ufisadi hadharani, kubuni njia na mikakati ya kukabiliana nao na kung'oa mizizi ya ufisadi katika serikali na mashirika ya biashara.

Akihutubia kikao hicho Rais wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim ametilia mkazo ulazima wa kupambana na ufisadi kivitendo na kubainisha kuwa unahitajika utekelezaji wa kivitendo katika nchi husika ili kuweza kuung'oa na kuutokomeza ufisadi. Kwa mujibu wa Rais wa Benki ya Dunia njia na mbinu za ufisadi zimekuwa tata zaidi kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia katika dunia ya kisasa.

Washiriki wa kikao cha kimataifa cha London cha kupambana na ufisadi wamekubaliana juu ya masuala kadhaa katika sura ya kifurushi cha mapendekezo, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kivitendo za kupambana na ufisadi ukiwemo wa ukwepaji kodi unaofanywa na mashirika ya kimataifa, kuwepo uwazi zaidi katika masuala ya kodi za serikali, kutilia mkazo utekelezaji wa sheria za kupambana na ufisadi na kuyapa nguvu zaidi mashirika ya kimataifa yanayosimamia ufisadi wa fedha. Katika kifurushi hicho cha mapendekezo imesisitizwa pia kuwepo mikakati ya kivitendo ya kuwachukulia hatua wahalifu na kuwasaidia waathiriwa wa vitendo vya ufisadi. Kabla ya kuanza kikao hicho, jopo la watu 300 linalojumuisha wataalamu wa uchumi na wahadhiri wa vyuo vikuu vya Uingereza liliwaandikia barua viongozi wa nchi washiriki kutaka zichukuliwe hatua kali za kupambana na ukwepaji kodi.

Katika kikao hicho cha London, Waziri Mkuu wa Uingereza ameweza kuzishawishi nchi kadhaa ikiwemo Kenya, Nigeria, Ufaransa, Afghanistan na Uholanzi zianzishe sheria itakayorahisisha urejeshaji fedha na mali. Mbali na hayo Cameron alitangaza hapo jana pia mkakati mpya wa serikali yake wa kupambana na utakatishaji fedha, uingizaji fedha haramu katika soko la mali na ukwepaji kodi kupitia uanzishaji mashirika hewa.

Kikao cha London kimefanyika katika hali ambayo kufichuliwa mamilioni ya nyaraka, maarufu kwa jina la "Panama Papers" za shirika la masuala ya sheria la Panama la Mossack Fonseca, kumeamsha hisia za fikra za walimwengu na nchi mbambali duniani juu ya ukwepaji kodi na ufisadi mkubwa wa fedha unaofanywa kwa sura na mbinu tofauti zikiwemo za utakatishaji fedha na ukwepaji kodi. Nyaraka hizo zinaonesha jinsi baadhi ya matajiri wakubwa na wenye satua kubwa duniani walivyoweza kuficha fedha na mali zao katika nchi na maeneo maarufu kwa ukwepaji kodi kwa kutumia mbinu tofauti ikiwemo ya kuasisi mashirika na makampuni hewa.../