Jeshi la Ufaransa lawataka wanajeshi walioandika barua ya kutokea mapinduzi wajiuzulu
(last modified 2021-05-12T11:08:14+00:00 )
May 12, 2021 11:08 UTC
  • Jenerali François Lecointre na Rais Macron
    Jenerali François Lecointre na Rais Macron

Mkuu wa Majeshi ya Ufaransa amewataka wanajeshi waliosaini barua inayotahadharisha kuhusu hatari ya kutokea vita vya ndani nchini humo wajiuzulu kutoka kwenye jeshi la nchi hiyo.

Wito huo wa Jenerali François Lecointre umetolewa baada ya majenerali wastaafu na baadaye maafisa wengine wa jeshi la Ufaransa kuandika barua mbili tofauti za wazi wakitahadharisha kuhusu uwezekano wa kutoka vita vya ndani na mapinduzi nchini humo.

Katika siku kadhaa zilizopita majenerali wastaafu na karibu maafisa 100 wa jeshi la Ufaransa walimwandikia barua ya wazi Rais Emmanue Macron wa nchi hiyo wakimtaka kukabiliana na kile walichodai ni hatari ya "Waislamu wenye misimamo mikali" la sivyo Ufaransa itatumbukia katika vita vya ndani.  

Jarida la Ufaransa la Le Point limeripoti kuwa: Baada ya barua iliyoandikwa tarehe 21 Aprili na majenerali wa jeshi la Ufaransa, kwa mara nyingine tena wanajeshi elfu mbili wa nchi hiyo wamewaandikia barua maafisa wa serikali ya Paris akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, mawaziri na wabunge wa nchi hiyo wakiunga mkono madai ya wanajeshi wenzao.

Mkuu wa majeshi ya Ufaransa Jenerali François Lecointre amewaambia maafisa wa jeshi waliounga mkono madai hayo kuwa mbinu ya kimantiki zaidi ya kueleza itikadi zao ni kujiondoa jeshini.

Uchunguzi wa maoni uliofanyika karibuni unaonesha kuwa, wananchi waliowengi wa Ufaransa wanaafikiana na barua ya majenerali wastaafu na maafisa wa jeshi waliotahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea mapinduzi na kujitosa uwanjani jeshi la nchi hiyo kwa ajili ya kudhibiti hali ya mambo.      

Tags