Iran ina azma ya kuwawezesha wanawake na wasichana
(last modified Fri, 22 Oct 2021 07:15:25 GMT )
Oct 22, 2021 07:15 UTC
  • Iran ina azma ya kuwawezesha wanawake na wasichana

Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina azma ya kufanya kilicho dharura ili kuwawezesha wanawake na wasichana."

Bi. Zahra Ershadi Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameyasema hayo Alhamisi wakati wa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambacho kiliitishwa kujadili wanawake, amani na usalama. Balozi Ershadi ameongeza kuwa, pamoja na kuwepo hatua zilizo jaa uhasana na zilizo kinyume cha sheria, yaani vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambavyo vimekiuka haki za kimsingi za wanawake na watoto, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina azma imara ya kuchukua hatua zinazotakiwa ili kuwawezesha wanawake na wasichana kuwa na nafasi muhimu katika jamii. 

Amesema wasichana na wanawake ndio ambao hupata madhara mabaya zaidi wakati wa vita na malumbano na kuongeza kuwa, Baraza la Usalama linapaswa kuchukua hatua za kulinda usalama na amani kimataifa ili kuwalinda wanawake na watoto.

Mkutano huo ulianza kwa kutazamwa video mahsusi inayoonesha jinsi wanawake walivyo mstari wa mbele kwenye ujenzi wa amani katika nchi zao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Balozi Raychelle Omamo wakitembelea maonyesho ya "Wanawake wachukua usukani wa amani" katika makao makuu ya UN New York

Kisha rais wa kikao ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Balozi Raychelle Omamo akaitisha kikao. Kenya ni mwenyekiti wa mzunguko wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi huu wa Oktoba.

Baada ya hapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akahutubia akisema ushiriki wa wanawake kama hao unazidi kukumbwa na changamoto kubwa ambapo katika baadhi ya nchi kama vile Afghanistan na Mali fursa hiyo imebinywa na kwingineko ushiriki wao hata kule ambako Umoja wa Mataifa unaendeleza shughuli za ulinzi na ujenzi wa amani unakumbwa na changamoto na vitisho. 

 

Tags