Uingereza yatenga bajeti ya dharura kukabiliana na ongezeko la wafungwa wanaojiua
https://parstoday.ir/sw/news/world-i7744-uingereza_yatenga_bajeti_ya_dharura_kukabiliana_na_ongezeko_la_wafungwa_wanaojiua
Uingereza imeamua kutenga bajeti ya dharura ya pauni milioni 10 kukabiliana na ongezeko la wafungwa wanaojiua na matatizo ya kiakili katika jela za nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 24, 2016 11:52 UTC
  • Uingereza yatenga bajeti ya dharura kukabiliana na ongezeko la wafungwa wanaojiua

Uingereza imeamua kutenga bajeti ya dharura ya pauni milioni 10 kukabiliana na ongezeko la wafungwa wanaojiua na matatizo ya kiakili katika jela za nchi hiyo.

Bajeti hiyo ya dharua imeidhinishwa na Waziri wa Sheria Michael Gove, kutokana na wasiwasi mkubwa uliopo kufuatia kuongezeka kwa kiwango kikubwa cha matukio ya wafungwa wanaojiua, wenye maradhi ya akili, matatizo ya hasira na chuki pamoja na mapigano baina ya wafungwa hao katika jela za nchi hiyo.

Ripoti zinaeleza kuwa wakuu wa jela za Uingereza watatumia bajeti hiyo kwa ajili ya ununuzi wa vifaa zaidi zikiwemo kamera za kurekodi matukio ili kufuatilia kwa karibu zaidi nyendo za wafungwa pamoja na uajiri na utoaji mafunzo kwa wafungwa hao.

Kwa mujibu wa Waziri wa Sheria wa Uingereza, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imetokea mikasa zaidi ya 100 ya wafungwa kujiua na ongezeko la matukio ya mapigano na kujeruhiana katika jela za nchi hiyo, ambayo ni hali inayotia wasiwasi mkubwa.

Katika barua aliyoiandikia kamati ya vyombo vya mahakama ya Bunge, Waziri wa Sheria wa Uingereza ametahadharisha juu ya kushadidi matatizo katika jela za nchi hiyo na kusisitiza juu ya udharura wa kufikiria njia za haraka za kutatua matatizo hayo.../