Marabi wa Kiyahudi wanaoipinga Israel wapeperusha bendera za Palestina nchini Marekani
(last modified Sat, 30 Apr 2022 08:19:37 GMT )
Apr 30, 2022 08:19 UTC
  • Marabi wa Kiyahudi wanaoipinga Israel wapeperusha bendera za Palestina nchini Marekani

Marabi wa Kiyahudi wa dhehebu la Orthodox wanaunga mkono vuguvugu la kuipinga Israel la "Neturei Karta" wameadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds kwa kupeperusha bendera ya Palestina mjini New York, Marekani.

Jumuiya ya Kimataifa ya Mayahudi "Neturei Karta" ilitoa taarifa jana katika Siku ya Kimataifa ya Quds ikisema: "Tunadhihirisha mshikamano wetu kamili na watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kulaani kikamilifu jinai zote zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina".

Taarifa hiyo imesema: “Kwa miaka 74 sasa, wananchi wa Palestina wamefukuzwa makwao, wamekandamizwa, kuuawa na kuporwa; Uvamizi huo haramu unaendelea hadi leo, hususan kwa mashambulizi ya mabomu huko Gaza, mauaji ya wanaume, wanawake na watoto, upanuzi unaoendelea wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, uharibifu wa nyumba na vitendo vya kichochezi vya hivi karibuni zaidi katika Msikiti wa Al-Aqsa.

Maandamano hayo ya Siku ya Kimataifa ya Quds yalihudhuriwa na idadi kubwa ya Waislamu waliofunga swaumu, mashirika ya kiraia na mashirika ya kutetea haki za binadamu, na wanaharakati wa Kiyahudi wanaopinga Uzayuni (Neturei Karta) huko Manhattan, New York.

Wakiwa wameshikilia mabango yenye ujumbe wa kuwaunga mkono watu wa Palestina, washiriki yamesisitiza udharura wa kukombolewa Palestina na Quds Tukufu, kibla cha kwanza cha Waislamu na ardhi takatifu ya dini za Mwenyezi Mungu.

Maandishi ya mabango hayo yalisomeka: "Palestina Ikombolewe", "Dhulma unapokuwa sheria, mapambano yanakuwa wajibu" na "Zuia mauaji ya watu wasio na hatia yanayofanywa Marekani na Israel." 

Tags