Oct 24, 2022 12:32 UTC
  • Mashariki mwa Ulaya inakabiliwa na janga la ufukara wa nishati na hewa chafu

Gazeti moja la Uingereza limeandika kuwa, wananchi wa maeneo ya mashariki mwa Ulaya wana utajiri mkubwa wa nishati ya bei nafuu lakini unasababisha uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa. Utajiri huo ni kama ule wa makaa ya mawe ya rangi ya kahawia.

Gazeti la Financial Times la Uingereza limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wananchi kama wa Hungary, wana utajiri mkubwa wa makaa ya mawe ya kahawia, kuni na vitu vingine vya kuzalisha nishati lakini vyote hivyo vinasababisha uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa.

Zoltán Berky, mmoja wa wananchi wa Hungary anasema, amelazimika kuchoma gogo la mti na viatu vyake vya michezo kwa ajili ya kupata joto ndani ya nyumba yake.

Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Mihály Orbán ameondoa masharti mengi ya kutumia magogo ya miti kama kuni na ameamrisha uzalishaji mkubwa zaidi wa makaa ya mawe ya kahawia licha ya kwamba makaa ni katika mada zinazochafua mno mazingira na hali ya hewa.

Msimu wa baridi kali umeziweka nchi za Ulaya kwenye mgogoro mkubwa baada ya zenyewe kuiwekea vikwazo Russia

 

David Mith, mtaalamu wa masuala ya Hungary katika Benki ya Ubelgiji ya KBC amesema kuwa, kama bei za bidhaa za kimsingi zitaendelea kuathiriwa na ughali wa nishati, basi watu wanaoishi kwenye umaskini hivi sasa watakuwa maskini zaidi katika siku za usoni.

Amesema, hivi sasa kipato cha Euro 500 kwa mwezi si pesa, kwani hazimfikishi popote mtu, na hazitoshi kununulia hata kuni za kutia joto kwenye nyumba za kawaida. Sababu yake ni kuwa, kila mita cubic moja ya kuni katika baadhi ya maduka makubwa ya Hungary inauzwa kwa zaidi ya Euro 200 na kiwango hicho cha kuni hakitoshi kutia joto hata katika nyumba ndogo tu kwa mwezi. Hii pia inaonesha ni kwa kiwango gani suala la kulindwa mazingira lilivyotupiliwa mbali na serikali nyingi za Ulaya.

Tags