Oct 26, 2022 07:37 UTC
  • IOM: Idadi ya vifo vya wahajiri kuelekea Ulaya imeongezeka zaidi mwaka huu

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kwamba idadi ya vifo vya watu wanaotafuta hifadhi imeongezeka kwa kiasi kikubwa kwenye njia za nchi kavu na baharini kuelekea Ulaya ikilinganishwa na mwaka jana.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza mjini Berlin kuwa watu wasiopungua 5,684 wamefariki dunia wakijaribu kukimbilia Ulaya kati ya Agosti 2021 na Septemba mwaka huu.

Ripoti ya IOM imesema, kufikia Agosti 2021, takriban watu 2,836 walikuwa wameaga dunia au kutoweka katika Bahari ya Mediterania. Katika kipindi cha 2019/2020, shirika hili lilikuwa limesajili watu 2262 walikuwa wamefariki dunia na kutoweka kwenye njia hiyo.

IOM imehusisha ongezeko la vifo vya wakimbizi na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kushindwa kimuundo kutayarishwa njia salama kwa wanaotafuta hifadhi.

Ukinukuu ripoti kutoka kwa walionusurika, Umoja wa Mataifa umesema watu wasiopungua 252 wanaaminika kufariki dunia kutokana na kile kinachoitwa mpango wa kuwarudisha nyuma wakimbizi unaotekelezwa na walinzi wa mpaka wa Ulaya. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UN, vifo vingi zaidi vya wakimbizi vimetokea Mediterania ya kati (97), mashariki mwa Mediterania (70) na kwenye mpaka kati ya Ugiriki na Uturuki (58).

IOM imesema, zaidi ya watu 29,000 wamekufa maji wakijaribu kukimbilia Ulaya tangu kuanza ukusanyaji wa takwimu hizo.

Tags