Nov 03, 2022 02:29 UTC
  • IEF: Bei ya mafuta kupindukia dola 100 kwa pipa

Jukwaa la Kimataifa la Nishati (IEF) limesema bei ya mafuta itapindukia dola 100 kwa pipa kutokana na utekelezaji wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia.

IEF ilisema hayo jana Jumatano na kuongeza kuwa, kutekelezwa vikwazo vya EU dhidi ya Russia kutapunguza usambazaji wa mafuta ya Moscow katika soko la dunia kwa mapipa kati ya milioni moja na milioni tatu.

Nchi za Ulaya zimeiwekea vikwazo Moscow kwa kisingizio cha vita vya Ukraine na kuiunga mkono serikali ya Kyiv, lakini hivi sasa kuna upungufu mkubwa wa nishati barani Ulaya na bei zinazidi kupaa kila uchao.

Jukwaa la Kimataifa la Nishati lenye makao yake mjini Riyadh limefafanua kuwa: Iwapo vikwazo vya Umoja wa Ulaya vitaanza kutekekelezwa mwezi ujao, bei ya mafuta katika soko la dunia litafikia dola 100 kwa pipa kiwepesi.

Weledi wanautazama mgogoro wa nishati Ulaya kama 'mwiba wa kujichoma'

Wananchi wa nchi nyingi za Ulaya wamekuwa wakifanya maandamano katika siku za hivi karibuni kulalamikia gharama ya juu ya maisha, huku wakishinikiza kutafutia ufumbuzi mgogoro wa nishati.

Ripoti za wataalamu wa masuala ya kiuchumi zinasema kuwa, mfumuko wa bei katika ukanda wa Euro umeongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, huku bei za vyakula zikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 katika kipindi cha mwezi mmoja. Mgogoro kama huo haujawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hizo za Ulaya.

 

Tags