WHO yatahadharisha juu ya madhara ya mafuriko nchini Pakistan
Shirika la Afya Duniani WHO kwa mara nyingine tena limetahadharisha kuhusu tishio la kiafya katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko huko Pakistan.
Pakistan mwaka huu imeathiriwa na mvua kubwa za masika kuwahi kushuhudwa nchini humo ambazo zimeuwa watu zaidi ya 1,700 wakiwemo watoto 647 na kupelekea wengine milioni 33 kukosa makazi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nyumba milioni mbili na shule 2700 zimebomolewa kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Pakistan.
Jumla ya watu milioni 9 huko wanakabiliwa na umaskini huko Pakistan kutokana na kupoteza ajira, mifugo yao, mavuno ya kilimo, nyumba, kufungwa shule,kuenea magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na pia kupanda kwa bei za vyakula kufuatia janga hilo la mafuriko.

Shirika la Afya Duniani limetangaza kuwa, hata kama katika wiki za karibuni mafuriko yamepungua katika maeneo mengi huko Pakistan lakini bado karbu watu milioni nane wanahitaji huduma za afya na tiba nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya WHO, watu zaidi ya 540,000 wameugua malaria huko Pakistan huku Idadi inayoongezeka ya magonjwa ya kuhara, homa ya dengue, surua na diphtheria yakishuhudiwa nchini humo kufuatia mafuriko hayo.