Maandamano makubwa ya Wafaransa ya kupinga sera za NATO na Ulaya katika vita vya Ukraine
(last modified Thu, 22 Dec 2022 03:08:51 GMT )
Dec 22, 2022 03:08 UTC
  • Maandamano makubwa ya Wafaransa ya kupinga sera za NATO na Ulaya katika vita vya Ukraine

Kutokana na kushamiri hali mbaya ya kiuchumi katika nchi mbalimbali za Ulaya, wananchi wengi wa nchi hizo wanapinga sera za Umoja wa Ulaya katika vita vya Ukraine. Hali mbaya ya uhaba wa nishati na wasiwasi unaotokana na msimu wa baridi kali unaokaribia kuanza,

kuongezeka gharama za maisha, kupanda kwa kodi na kutokuwapo na uhakika wa hali itakavyokuwa katika siku zijazo vimewafanya raia wa nchi mbalimbali za Ulaya waamue kuitisha maandamano ya upinzani kushinikiza serikali zao zikomeshe uungaji mkono wao kwa Ukraine katika vita dhidi ya Russia.

Kuhusiana na hilo, mapema wiki hii mitaa na barabara za mji mkuu wa Ufaransa, Paris ilishuhudia maandamano makubwa ya hadhara ya kupinga sera za serikali kuhusiana na Ukraine na uwanachama wa nchi hiyo katika shirika la kijeshi la NATO.

Maandamano makubwa ya kupinga NATO Ufaransa

Katika maandamano hayo makubwa ambayo yalikuwa yameandaliwa na chama cha siasa za mrengo wa kulia cha Wazalendo, Les Patriots (The Patriots), kinachoongozwa na Florian Philippe, naibu wa zamani wa chama cha National Movement cha Marine Le Pen, kiongozi huyo wa upinzani alitaka Ufaransa ijitoe katika shirika la kijeshi la NATO na Umoja wa Ulaya.

Tokea miezi kadhaa nyuma, hali ya kiuchumi na kijamii imezidi kuwa mbaya katika nchi nyingi za Ulaya, na ingali inaendelea kuwa hivyo hadi sasa. Kwa hakika sera za uingiliaji za nchi za Ulaya na kufuata kwao matakwa ya Marekani ya kujiingiza katika kadhia ya vita vya Ukraine kumeifanya hali ya mambo katika nchi za Ulaya iwe ngumu mno, na hivi sasa serikali za nchi hizo zinakabiliwa na maandamano ya kijamii, matatizo ya kiuchumi na kushamiri vyama vya mrengo wa kulia na vyenye misimamo mikali katika nchi hizo. Kuhusiana na hilo, Ujerumani na Ufaransa, nchi mbili muhimu za Umoja wa Ulaya na ambazo siku zote zimeonekana kuwa na uchumi imara na hivyo kuathiri maamuzi ya Umoja wa Ulaya katika masuala mbalimbali, hivi sasa zinakabiliwa na hali ya aina yake.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Hata kama katika miaka ya karibuni Ufaransa imeshuhudia vuguvugu la upinzani linalojulikana kama “Vizibao vya Njano”, ambayo ni harakati inayopinga mfumo wa kibepari nchini Ufaransa na sera za serikali ya Rais Emanuel Macron, lakini katika miezi ya karibuni na kufuatia kuongezeka bei za bidhaa za nishati, kupanda kwa bei za vyakula, kuongezeka ughali wa maisha, ukosefu wa ajira na kupungua ukuaji wa uchumi, raia wa Ufaransa wamezidi kuwa wakosoaji wa sera za serikali ya nchi hiyo.

Kwa mtazamo wa raia wengi wa Ufaransa, ushiriki wa nchi hiyo katika vita vya Ukraine na kutengwa bajeti kubwa ya msaada wa kifedha na kijeshi kwa ajili ya Kyiv, na vilevile kushiriki katika NATO na kuchangia gharama zinazohusiana na vita hivyo, ambazo zote hizo zinatoka mifukoni mwa raia wa Ufaransa ni sera mbovu inayotekelezwa na rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron. 

Marine Le Pen, kiongozi wa mrengo uitwao Mjumuiko wa Kitaifa katika Bunge la Ufaransa, ametaka kusitishwa misaada ya kijeshi ya nchi hiyo kwa Ukraine, ambayo inadhoofisha akiba ya silaha za Ufaransa, akisema: "msaada kwa Ukraine usiwe sababu ya kusababisha madhara kwa usalama wa taifa wa Ufaransa. Kutoa silaha nzito ambazo jeshi la Ufaransa linazihitaji maana yake ni kudhoofisha usalama wa taifa wa Ufaransa".

Silaha za kisasa inazopatiwa Ukraine na nchi za Magharibi

Kwa hakika nchi za Ulaya hivi sasa zinaendelea kutoa misaada kwa Ukraine huku raia wa Ulaya wakikabiliwa na dhiki ya kifedha na kiuchumi, na kwa kweli kuendelezwa sera hiyo kunaonyesha jinsi viongozi wa Ulaya wasivyoheshimu madai na kauli mbiu zao wanazotoa kama kujenga demokrasia na kuheshimu haki za watu na haki za kiraia ambazo wamekuwa wakizipigia upatu kwa miaka mingi.

Kwa upande mwingine, kutuma zana za kijeshi huko Ukraine kunaonyesha utegemezi wa nchi za Ulaya kwa sera ya kushupalia vita ya Marekani na kudhihirisha kwamba madai ya Ulaya ya kukemea na kuchukia vita ni porojo tupu.

Kuhusiana na hilo, Etriot Florian Philippe, kiongozi wa vuguvugu la Wazalendo wa Ufaransa, amekosoa upelekaji silaha Ukraine unaofanywa na Ufaransa na kuandika: "akiba ya silaha ya Ufaransa inakaribia kumalizika, lakini utumaji wa silaha na zana za kivita kwa Kyiv ungali unaendelea. Lazima msimamishe kikamilifu hatua hii ya kiwendawazimu". 

Madaktari, wanasheria, wafanyakazi wa reli na wa sekta nyingine nyingi za ajira nchini Ufaransa wametangaza kuwa wataendeleza maandamano yao ya upinzani. Vyama vya wafanyikazi pia vimesisitiza kuwa vitafanya maandamano mapya kuanzia Januari 2023 ikiwa serikali haitatimiza matakwa yao.

Inavyoonekana, mgogoro huo unaendelea kupanuka zaidi kuliko viongozi wa Ulaya na hasa wa Ufaransa wanavyodhani; na iwapo serikali za Ulaya na Ufaransa hazitakidhi matakwa ya wananchi, uthabiti wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo na Ulaya utakabiliwa na hatari kubwa.../

 

 

Tags