Pervez Musharraf, rais wa zamani wa Pakistan afariki dunia
(last modified Sun, 05 Feb 2023 10:34:28 GMT )
Feb 05, 2023 10:34 UTC
  • Pervez Musharraf, rais wa zamani wa Pakistan afariki dunia

Pervez Musharraf, rais wa zamani wa Pakistan amefariki dunia katika Umoja wa Falme za Kiarabu akiwa na umri wa miaka 79.

Vyombo vya habari huko Imarati na Pakistan vimenukuu watu wa familia ya Musharraf wakithibitisha habari ya kutokea kifo cha jenerali huyo wa zamani wa jeshi la Pakistan.

Rais huyo wa zamani wa Pakistan ambaye alienda uhamishoni yeye mwenyewe huko UAE, alikuwa amelazwa hospitalini kwa miezi kadhaa mjini Dubai, akitibiwa ugonjwa wa Amyloidosis ambao unaathiri viungo vya mwili kama vile moyo, figo, mfumo wa neva.

Shazia Siraj, msemaji wa ubalozi mdogo wa Pakistan mjini Dubai na ubalozi wa nchi hiyo mjini Abu Dhabi amethibitisha habari za kuaga dunia Musharraf.

Pervez Musharraf aliingia madarakani mwaka 1999 kupitia mapinduzi ya kijeshi na akaitawala Pakistan kwa muda wa miaka tisa kabla ya kuondolewa uongozini wakati chama chake kiliposhindwa katika uchaguzi mkuu.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2019, Mahakama maalumu ya Pakistan ilimhukumu adhabu ya kifo rais huyo wa zamani wa nchi hiyo baada ya kumpata na hatia ya kutenda kosa kubwa la uhaini na kukiuka katiba ya nchi.

Musharraf (kulia) akitibiwa hospitalini Dubai

Kesi ya uhaini dhidi ya Pervez Musharraf, iliyotokana na hatua aliyochukua tarehe 3 Novemba, 2007 ya kutangaza hali ya hatari nchini, ilianza kusikilizwa mwaka 2014. Kufuatia hatua yake hiyo ya kutangaza hali ya hatari, jenerali huyo mstaafu wa jeshi la Pakistan alisimamisha katiba na kuwaweka kizuizini wanasiasa waandamizi na majaji.

Mgogoro huo ulichochewa na jaribio lililofanywa na Musharraf mnamo mwezi Machi mwaka 2007 la kumwachisha kazi Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Pakistan wakati huo Iftikhar Muhammad Chaudhry, uamuzi ambao ulikuja kutenguliwa na kubatilishwa na Mahakama ya Juu Kabisa ya nchi hiyo.