Mahakama Pakistan yaamuru waziri mkuu wa zamani Imran Khan akamatwe
Feb 28, 2023 10:05 UTC
Mahakama ya Islamabad imetoa waranti wa kukamatwa waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Imran Khan.
Kesi inayomkabili Imran Khan, waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, inahusiana na shutuma za matumizi mabaya ya hazina ya serikali. Imran Khan kwa sasa yuko Islamabad, mji mkuu wa Pakistan kuhudhuria kikao cha mahakama kinachohusiana na kesi kadhaa za ukiukaji sheria zinazomkabili.
Kwa sababu hiyo, vyombo vya habari vya Pakistan vimesema kuna uwezekano wa waziri mkuu huyo wa zamani wa nchi hiyo kutiwa nguvuni na vyombo vya usalama.
Kabla ya hapo,Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Pakistan na kituo kimoja cha polisi mjini Islamabad nazo pia zilikuwa zimetoa waranti wa kutiwa nguvuni Imran Khan.
Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB limekinukuu kituo cha habari cha Ham News kikiripoti kuwa, mahakama ya Islamabad, mji mkuu wa Pakistan, leo Jumanne imeamuru kukamatwa Imran Khan, waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, wakati ilipokuwa ikichunguza faili la kesi ya rushwa na matumizi mabaya ya Hazina ya Taifa.
Kulingana na vyanzo vya habari, hukumu iliyotolewa ya kukamatwa Imran Khan haiwezi kuakhirishwa kwa dhamana na lazima itekelezwe. Kwa sababu hiyo ripoti zinasema wafuasi wa chama cha Tehreek-e-Insaf kinachoongozwa na waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan wamekusanyika mbele ya mahakama na maeneo mengine ya mji wa Islamabad kulalamikia uamuzi huo wa mahakama.
Kabla ya hapo Imran Khan, alipatiwa kinga ya mahakama mara kadhaa kufuatia tukio la kushambuliwa kwa kupigwa risasi na kujeruhiwa mguuni.../
Tags