Jun 19, 2023 13:11 UTC
  • Safari ya kwanza ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani nchini China baada ya miaka mitano

Anthony Blinken Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Jumapili ya jana tarehe 18 Juni aliwasili Beijing mji mkuu wa China, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza mvutano unaoongezeka kati ya nchi mbili hizo ambao umezitia wasiwasi nchi nyingi.

Blinken ndiye afisa wa ngazi za juu wa Marekani kuzuru China tangu Rais Joe Biden aingie madarakani, na pia ni waziri wa kwanza wa mambo ya nje wa Marekani kuzuru China katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Blinken alisema Ijumaa kuwa Joe Biden na Xi Jinping wameahidi kuboresha mahusiano "ili tuweze kuwasiliana kwa uwazi iwezekanavyo na hivyo kuzuia  hali tarajiwa ya suitafahamu na kutoelewana."

Safari hii ya siku mbili inakuja baada ya safari ya Blinken iliyopangwa hapo awali mwezi Februari kucheleweshwa kufuatia kutunguliwa kwa puto la China la uchunguzi katika anga ya Marekani.

Muda mfupi kabla ya kuondoka kuelekea China, Blinken alisisitiza umuhimu wa kujenga na kudumisha njia bora za mawasiliano kati ya Marekani na China. Blinken alisema, Marekani inataka kuhakikisha kuwa "ushindani tulionao na China hauingii kwenye migogoro kwa sababu ya suitafahamu zinazoweza kuepukika."

Safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani nchini China inafanyika sambamba na juhudi jumla ingawa za kidhahiri za serikali ya Biden kuzuia kushtadi kwa mvutano kati yake na China na kuunda njia ya mawasiliano kati ya nchi hizo mbili ili kuepusha suitafahamu inayoweza kutokea na kuongezeka mvutano kati ya Washington na Beijing.

Kabla ya hapo, maafisa waandamizi wa China walikuwa wametoa jibu hasi kwa ombi la wenzao wa Marekani la kufanyika mkutano wa pande mbili na kulihesabu hilo kama radiamali za hatua za chuki na hasama za Washington na misimamo hasi ya viongozi wa White House dhidi ya Beijing. Pamoja na mambo mengine, Waziri wa Ulinzi wa China Li Shangfu alikataa kukutana na mwenzake wa Marekani Lloyd Austin kando ya mkutano wa usalama wa Shangri-La huko Singapore mwanzoni mwa mwezi Juni, au hata kumpa mkono, kwa sababu Washington imekataa kuondoa vikwazo dhidi yake.

Image Caption

 

Licha ya Austin kusisitiza kwamba,  mazungumzo kati ya Marekani na China ni ya lazima na yatasaidia kuepuka makosa yanayoweza kusababisha mzozo, lakini kwa mara nyingine alisisitiza msimamo wa Washington ulio dhidi ya China na kudai kuwa Marekani haiwezi kuvumilia kile alichokiita kuwa “udhibiti na utumiaji mabavu” wa China. Waziri wa Ulinzi wa Marekani alisema: Ikulu ya Marekani White House na washirika wake wanaamini kuwa, njia bora ya kukabiliana na nguvu ya China ni kudhamini usalama wa Bahari ya Hindi na Pasifiki na kuanzisha Mashariki ya Mbali huru.

Kwa muda mrefu, Marekani imeitambua China kuwa tishio muhimu zaidi dhidi yake na ulimwengu wa Magharibi na kusisitiza ulazima wa kukabiliana na matarajio na mipango ya Beijing yenye malengo ya mbali. Wakati wa uzinduzi wa mkakati wa ulinzi wa kitaifa katika Pentagon mwishoni mwa Oktoba 2022, Lloyd Austin alibainisha kuwa, licha ya mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine, China bado ni tishio kubwa kwa Marekani.

Maafisa waandamizi wa jeshi na usalama wa serikali ya Biden wametangaza mara kwa mara kwamba, China ni changamoto muhimu zaidi ya kijiopolitiki kwa Marekani. Uundaji huu wa taswira wa Marekani chimbuko lake ni woga na hilo linaweza kutathminiwa kwa kuzingatia makabiliano yanayoongeza ya Beijing na Washington katika uga wa kieneo na kimataifa.

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, Washington inaogopa kwamba China, ikishirikiana na Russia, zisije zikautia dosari na kuupa changamoto mfumo wa kimataifa wa kiliberali, ambao ulimwengu wa Magharibi ndio muundaji na muungaji mkono wa kuendelea kuwepo kwake, na hivyo kudhoofisha mamlaka ya karne nyingi ya Magharibi kwa mfumo wa kimataifa.

Hapana saka kuwa,  kuendelea na kushadidi makabiliano kati ya Marekani na China hususan katika eneo la Asia Pacific kunaweza kuongeza hatari ya mzozo baina ya nguvu hizi mbili kubwa kimataifa.

Henry Kissinger, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na mwanastratejia mashuhuri wa Marekani, ametahadharisha katika matamshi yake ya hivi karibuni kwamba: Iwapo Marekani na China hazitaachana na misimamo yao na kulegeza kamba, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea Vita vya Tatu vya Dunia.

Tags