May 17, 2018 04:21 UTC
  • Alkhamisi, Mei 17, 2018

Leo ni Alhamisi tarehe Mosi Ramadhani 1439 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 17 Mei 2018 Miladia.

Leo ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria; mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qurani Tukufu. Ni mwezi wa rehema na baraka za kiroho. Katika kubainisha utukufu wa mwezi huu, Mtume Mtukufu SAW amesema, siku za mwezi huu ndizo siku bora zaidi kuliko siku nyingine zote na kuwataka Waislamu wachume na wafaidike kutokana na fadhila na baraka za kiroho za mwezi huu. Allah SWT anasema: ((Hakika tumeiteremsha (Qurani) katika usiku wa heshima. Na nini kitakujulisha usiku huo wa heshima ni nini? Laylatul Qadr (usiku huo wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu.))

Tukio la kuhuzinisha moyo la kuuawa shahidi Imam Ali AS na kuzaliwa Mjukuu wa Mtume SAW,  Imam Hassan AS,  ni katika matukio muhimu yaliyotimia katika mwezi huu. Tunamuomba Allah SW atupe baraka za kimaanawi za mwezi huu na kwa fadhila za mwezi huu mtukufu tuwe karibu na rehema na msahamaha Wake.

@@@@

Aidha siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kiliteremshwa kitabu cha Suhf cha Nabii Ibrahim AS. Jina Ibrahim limetajwa mara 69 katika Qur'ani Tukufu kwa heshima na taadhima ambapo maisha yake yameashiriwa kwa njia mbali mbali kama ibra na ruwaza njema kwa waumini. Mwenyezi Mungu amemtaja kuwa ni mtu mwenye kumuabdudu Mungu mmoja na dini imetajwa kuwa ya Hanifa katika aya ya 67 ya Sura Aal Imran na pia katika aya ya 125 ya Sura An Nisaa. Alikuwa Nabii mkweli kama tunavyosoma katika Surat Maryam aya ya 41. Aidha Mwenyezi Mungu alimpa yeye na familia yake neema na mamlaka kama tunavyosoma katika Surat An Nisaa aya ya 54.

Kuna vitabu kadhaa vya mbinguni ambavyo waliteremshiwa Mitume kama vile Suhf cha Ibrahim AS na Nuh AS, Taurati ya Musa AS na Injili ya Issa AS na kitabu kilicho kamilika kati ya vyote hivyo ni Qur'ani Tukufu.

@@@@

Katika siku kama ya leo miaka 1011 iliyopita alifariki dunia Ibn Sina maarufu kwa jina la Sheikhur Rais, tabibu, mtaalamu wa hisabati, falsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani. Ibn Sina alifariki dunia katika mji wa Hamadan ulioko magharibi mwa Iran akiwa na umri wa miaka 58. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana na akapata kusoma elimu za mantiki, uhandisi na utaalamu wa nyota. Baada ya kumtibu Nuh bin Mansur, mmoja wa Wafalme wa Kisamani akiwa kijana, Ibn Sina alipata idhini ya kutumia maktaba kubwa ya mfalme huyo. Katika maktaba hiyo, Ibn Sina alipata kusoma vitabu vingi vya elimu tofauti. Abu Ali Sina alitokea kuwa msomi, mwandishi na mtafiti mashuhuri. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha "Shifaa" kinachohusu elimu ya falsafa, "Qanun" kinachohusu tiba na "Daneshnameh Allai".

@@@

Siku kama ya leo miaka 707 iliyopita,  alizaliwa Ibn Khaldun, mtaalamu wa masuala ya kijamii, mwanasiasa na mwanahistoria Mwislamu. Ibn Khaldun alizaliwa huko Tunisia. Maisha ya Ibn Khaldun yanaweza kugawanywa katika sehemu tatu ambapo maisha yake ya awali aliyatumia katika kusoma elimu tofauti. Alitumia sehemu ya pili ya maisha yake katika siasa na kuhudumia nyadhifa tofauti za utendaji nchini ambapo kutokana na njama za maadui zake, alifungwa jela. Baada ya kuachiliwa huru Ibn Khaldun alijitenga na siasa. Hapo ndipo ilianza duru ya tatu ya maisha yake ambapo alijishughulisha na utafiti na uandishi. Alimu na msomi huyo alifariki dunia mwaka 808 Hijiria. ***

@@@

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, dola la Uingereza ambalo Palestina ilikuwa chini ya mamlaka yake, lilitoa kitabu kwa jina la The White Paper  "Kitabu Cheupe" na hivyo kukawa kumepigwa hatua nyingine katika njia ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel. Wapalestina ambao walikuwa wakifahamu vyema himaya ya Uingereza kwa Wazayuni, waliukataa mpango uliokuwa umependekezwa katika kitabu hicho kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.

@@@

Miaka 153 iliyopita katika siku kama ya leo, ulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kimataifa katika uwanja wa mwasiliano huko Paris Ufaransa. Utiaji saini huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 20 duniani. Kwa utaratibu huo kukawa kumepasishwa hati ya kuasisiwa Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana siku hii ikapewa jina la Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano. Mwaka 1932 kwa mujibu wa maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa Madrid Uhispania, jina la Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu au Internatioanl Telegraph Union lilibadilishwa na kuwa, Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano au  International Telecomunication Union (ITU) na vipengee pamoja na sheria za jumuiya hiyo zikapitiwa upya. Kuanzia mwaka 1947, taasisi hiyo ikawekwa rasmi katika faharasa ya asasi zilizoko chini ya Umoja wa Mataifa.

@@@

Katika siku kama ya leo miaka 9 iliyopita yaani tarehe 27 Ordibehesht 1388 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Bahjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najaat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo. ***