Sep 17, 2022 04:23 UTC
  • Jumamosi, 17 Septemba, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Tano Safar 1444 Hijria sawa na tarehe 17 Septemba 2022.

Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali (as) na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala. ***

 

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita, alizaliwa Ayatullah al-Udhma Mar’ashi Najafi mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Najaf nchini Iraq. Baba yake ni Sayyid Shamsuddin Mahmoud Mar’ashi aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na mafaqihi wakubwa katika zama zake. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na ya Kiislamu huko Najaf, Mar’ashi Najafi alianza kuhudhuria darsa na masomo ya Usul kwa Agha Dhiyau Iraqi na Sheikh Ahmad Kashif al-Ghitaa. Ayatullah Mar’ashi Najafi alipata daraja ya juu ya elimu yya Ij’tihad akiwa na umri wa miaka 27. ***

Ayatullah Mar'ashi Najafi

 

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, aliaga dunia Emil Ludwig mwandishi wa wasifu wa Kijerumani. Alizaliwa 1881 katika mji wa Breslau nchini Ujerumani ambao leo hii ni sehemu ya ardhi ya Poland. Alipata umashuhuri katika nusu ya pili ya karne ya 19 baada ya kuandika wasifu wa Otto Van Bismarck Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, kiongozi wa zamani wa Russia Joseph Stalin, Beethoven na rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Ludwig alikuwa mwandishi wa habari aliyepata nafasi ya kufanya mahojiano na watawala waliokuwa na satua na ushawishi mkubwa katika kipindi hicho kama Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchil na Joseph Stalin. ***

Emil Ludwig mwandishi wa wasifu wa Kijerumani

 

Tarehe 17 Septemba miaka 61 iliyopita aliuawa waziri mkuu wa zamani wa Uturuki, Adnan Menderes. Alizaliwa mwaka 1899 na kupata elimu katika taaluma ya sheria. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa bado kijana na alishika hatamu za uongozi nchini Uturuki kama waziri mkuu mwaka 1950. Menderes ambaye alikuwa akifuata siasa za sera za kimarekani, alituma vikosi vya jeshi kushambulia Wakurdi wa nchi hiyo, suala ambalo liliwakasirisha sana wasomi na wanafikra wengi nchini Uturuki. Mwaka 1957 alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Uturuki na kukandamiza maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakipinga utawala wake na kudai marekebisho ya kisiasa. Mwaka 1960 Adnan Menderes aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kufikishwa mahakamani ambapo alihukumiwa kifo kwa kupatikana na hatia ya kuua wanafunzi wa vyuo vikuu, kukiuka katiba ya nchi na kuwa na mahusiano haramu. Usiku wa kutekelezwa hukumu ya kifo, Menderes alifanya jaribio la kujiua lakini madaktari waliwahi kuokoa maisha yake. Hatimaye tarehe 17 Septemba, Adnan Menderes alinyongwa akiwa na umri wa miaka 62.

Adnan Menderes

 

Na tarehe 26 Shahrivar miaka 42 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, utawala wa zamani wa Iraq ulifuta kwa upande mmoja makubaliano ya mipaka ya mwaka 1975 yaliyojulikana kwa jina la Mkataba wa Algeria kati yake na Iran. Siku hiyo, Saddam Hussein kiongozi wa zamani wa Iraq aliuchana mkataba huo wa Algeria mbele ya kamera za televisheni akiungwa mkono na madola ya kibeberu. Mkataba huo wa mwaka 1975 wa Algeria yalikuwa makubaliano ya mwisho kati ya nchi hizo mbili kwa ajili ya kutatua hitilafu za mipaka. Siku kadhaa baadaye, Saddam Hussein alianzisha uvamizi wa miaka minane dhidi ya ardhi ya Iran kwa uchochezi wa nchi za Magharibi. ***

 

Tags