Dec 05, 2022 06:55 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (47)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 47 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia maudhui yenye umuhimu mkubwa ya "Kujitawala Kisiasa". Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Miongoni mwa masuala muhimu sana na ya msingi katika utamaduni wa kisiasa wa Uislamu ni "kujitawala na kujitegemea kisiasa". Kutokana na tofauti na mgongano wa kimitazamo uliopo kati ya mfumo wa kisiasa wa Uislamu halisi wa asili na mifumo ya kisiasa ya Ubeberu na Uistikbari wa dunia, ambayo kitu pekee inachojali ni kuyaburuza na kuyatwisha mataifa na nchi zingine matakwa na mitazamo yao, utamaduni wa kitauhidi wa Uislamu, unapinga ubeberu na kutoridhia kuburuzwa na kunyongeshwa kwa namna yoyote ile; na badala yake unaupa msukumo na ilhamu umma wa Kiislamu ya kupigania kujitawala na kujitegemea. Chimbuko la mtazamo huu ni kitabu cha mbinguni na kitukufu cha Qur'ani ambacho katika sehemu ya mwisho ya aya ya 141 ya Suratu-Nisaa kinasema: "…wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini".

Kwa muktadha huo, kuridhia unyongeshwaji wa aina yoyote ile hakuendani na dhati ya Tauhidi na kwa mtazamo huo tunaweza kubaini sura halisi ya tawala ambazo kidhahiri zinaonekana na zinajifanya kuwa ni za Kiislamu, lakini kinyume na maamrisho ya dini zimeridhia na zinaendelea kuridhia kunyongeshwa na kudhalilishwa na ukafiri duniani. Kwa hakika tawala za aina hiyo ni kama hazijasikia wala kunusa hata harufu ya Uislamu na mafundisho sahihi ya Tauhidi, kwa sababu kutokana na kujali kulinda nafasi na maslahi yao, watawala wake sio tu wanawakumbatia viongozi na watawala wa Marekani, Ulaya na Uzayuni wa kimataifa, lakini kutokana na kuwauzia pia mafuta na kununua kwao silaha za kisasa kwa mabilioni ya dola, wanaanzisha vita angamizi dhidi ya mataifa huru kama Yemen, Syria na Iraq na wala hawasiti kuyatendea jinai za aina yoyote ile mataifa hayo.

Ili kuweza kupata ufahamu na uelewa mpana zaidi kuhusu misingi ya kitauhidi ya utamaduni wa kujitawala na kujitegemea kisiasa, tuitalii kwa pamoja miongozo ya Imam Ali AS inayotoka kwenye chemchemi ya fikra halisi za kitauhidi. Mtukufu huyo anasema: "Kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu alimtuma na kumpa Utume kwa haki Nabii Muhammad SAW ili awatoe waja wake kwenye utumwa wa kutii na kuabudu (madhihirisho ya wenye nguvu na utajiri) na kuwaongoza kwenye ibada ya (Mungu mmoja pekee); kuwakomboa na mafungamano ya (kidhalimu) na kuwaweka kwenye mafungamano ya (kiuadilifu) ya Mwenyezi Mungu; kuwaepusha na kuwaweka mbali na utiifu (wa kibubusa na wa kuburuzwa na wanaotegemea nguvu); kuwalingania kumtii Mwenyezi Mungu kwa (basira na uelewa); kuwakataza kuwa na urafiki na kuukubali uongozi wa (watawala madikteta) na kuwaelekeza kwenye uwalii na utawala wa Mwenyezi Mungu Mwenye rehema na Mwenye hekima". (al Kafi 8/386)

Kwa maelezo haya inabainika kuwa, kujitegemea na kujitawala katika utamaduni wa kisiasa wa Uislamu halisi na wa asili, chimbuko lake liko kwenye mafundisho yenye maana nzito na ya kina ya mtazamo wa Tauhidi juu ya ulimwengu, mafundisho ambayo haipasi yakengeukwe katika hali na mazingira yoyote yale. Pamoja na maelezo tuliyotoa, ifahamike wazi kwamba, maana ya kujitegemea na kujitawala kisiasa si kukata mahusiano ya kisiasa kimataifa na nchi zingine; bali madhumuni yake ni kwamba, sambamba na kujenga uhusiano na kuheshimu ahadi na mikataba unayofungiana na nchi zingine, Ulimwengu wa Kiislamu uendelee kujitegemea na kujitawala katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni; na wala usije ukatoa mwanya wowote kwa wanyonyaji wa dunia kuyaburuza na kuyanyongesha mataifa ya Kiislamu. Katika aya ya mwanzo ya Suratul-Mumtahinah, Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla anawapa waumini angalizo ili wahakikishe umma wa Kiislamu hauji kunasa kwenye mtego huo aliposema: "Kwa jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu.  Enyi mlio amini! Msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa marafiki mkiwapa mapenzi, na hali wao wamekwisha ikataa haki iliyo kujieni, wakamfukuza Mtume na nyinyi kwa sababu mnamuamini Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu. Mnapotoka kwa ajili ya Jihadi katika Njia yangu na kutafuta radhi yangu, mnafanya urafiki nao kwa siri, na Mimi nayajua mnayo yaficha na mnayo dhihirisha. Na mwenye kufanya hayo kati yenu basi ameipotea njia ya sawa".

Lakini licha ya upambanuzi na mwongozo huu wadhiha na wa wazi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, yumkini baadhi ya watu wenye uelewa mdogo wakahoji, nini kitakachotutokezea endapo tutaridhia kuendeshwa na kuburuzwa na maajinabi wasio Waislamu? Katika aya ya pili ya sura hiyohiyo ya Mumtahinah, Qur'ani tukufu inajibu suali hilo kwa kusema: "Wakikuwezeni wanakuwa maadui zenu, na wanakukunjulieni mikono yao na ndimi zao kwa uovu. Na wanapenda muwe makafiri".

Kwa msingi huo, kujitawala na kujitegemea kisiasa ni suala lenye msukumo na kukubalika kiakili na pia kidini; na vilevile kunaweza kuupa nguvu na uwezo Ulimwengu wa Kiislamu wa kuufanya sio tu usijihisi katu kuwa duni, dhaifu, dhalili na usio na uwezo katika milingano na mahusiano ya kimataifa, lakini pia kuuwezesha kila mara kuwa na nguvu na uimara wa kukabiliana na maadui. Kitu kinachotoa ilhamu ya kuwa na uwezo huo ni aya ya 139 ya Suratu Aal Imran ambayo inawahutubu Waislamu ya kwamba: "Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini". 

Sababu moja muhimu inayoweza kudhoofisha moyo wa kujitawala na kujitegemea kisiasa ni kuyahofu madola ya kishetani. Kinachochochea mtazamo huo ni kutishika na makeke ya nguvu za madola machokozi ya kibeberu ambayo hujaribu kila mara kutumia nyenzo za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijeshi ili kuyanyongesha madola yanayodhulumiwa duniani na tawala vibaraka na zilizo dhalili kwa madola hayo ya kibeberu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameibatilisha dhana na mtazamo huo finyu na potofu alipoyafananisha madola hayo ya kibeberu na nyumba ya buibui kama aya ya 41 ya Suratul-Ankabut isemavyo: "Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua".

Matumaini yetu ni kwamba kwa mwamko, uelewa na juhudi za mataifa ya Waislamu na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu itafika siku ambapo tutakuja kushuhudia nguvu, kujitegemea na kujitawala Ulimwengu wa Kiislamu. Na kwa dua na tamanio hilo mpendwa msikilizaji, niseme pia kuwa sehemu ya 47 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 48 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/